Mwanasiasa Mkongwe Khamis Mgeja
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation na Mwanasiasa Mkongwe Nchini Khamis Mgeja amekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kudhihirisha ukomavu wa kuongoza nchi baada ya kukubali mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mgeja ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga amesema waliodai CCM haitaki kuendeleza mchakato wa katiba mpya walikuwa ni waongo, wazushi na wapotoshaji wakubwa wa chuki kwa umma.
“Hongera CCM imedhihirisha ukomavu wa kuongoza nchi na bado itaendelea kuongoza nchi kwa muda mrefu, kitendo cha CCM hivi karibuni kupitia kikao cha halmshauri kuu ya CCM taifa kuielekeza na kuishauri serikali ianze kuangalia namna bora ya kufufua muendelezo wa mchakato wa katiba mpya kwa maslahi mapana ya taifa kinaonesha ukomavu wa CCM”,amesema Mgeja.
Amesema maamuzi ya CCM kukubali mchakato wa upatikanaji katiba mpya ni kuwaumbua wale wote waliokuwa wanapotosha umma na kupandikiza chuki dhidi ya CCM, kuwa CCM haitaki kuona mchakato wa katiba unaendelezwa.
“Wana CCM na watanzania tuunge mkono maamuzi ya CCM yanayozingatia mahitaji ya wakati kwa maslahi mapana ya taifa na yanayohitaji kusubiri, tuwe na subira ni muhimu sana CCM iongoze mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwani ndio chama kilichoaminika kwa wananchi na kupewa dhamana ya kuongoza nchi”,ameongeza Mgeja.
Juni 21,2022 Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, itikadi na Uenezi (NEC) Shaka Hamdu Shaka alisema Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana kuwa upatikanaji wa Katiba Mpya na kwamba Chama hicho kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kuishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya watanzania wote.
Social Plugin