TANESCO KAGERA YAZINDUA RASMI MFUMO MPYA WA NI - KONEKT...SASA WATEJA KUPATA HUDUMA ZA UMEME KIDIGITALI

Baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco walioshiriki hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo mpya wa Ni-konekt
Baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco walio shiriki hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo wa Ni- konekt
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera akizungumza uzinduzi wa mfumo mpya wa Ni-konekt
Mteja wa kwanza kupata huduma ya umeme kwa mfumo mpya wa Ni-konekt Bi. Rosemary Peter akizungumza
Mkandarasi wa TANESCO Kagera Edwin Edward akizungumzia huduma ya Ni -konekt app ilivyo warahisishia kazi


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kagera limezindua rasmi mfumo wa Ni-konekt ambao mteja atatumia kupata huduma za umeme kwa njia ya simu yake ya mkononi au kifaa chochote chenye uwezo wa Intaneti.


Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla fupi ya uzinduzi huo katika ofisi za Tanesco Kagera leo Juni 6,2022 , Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera Mhandisi Godlove Mathayo amesema mfumo wa Ni-konekt utatumika kwa wateja wote wapya ambao watahitaji Huduma ya kuunganishiwa umeme katika maeneo yao ndani ya Mkoa wa Kagera na huduma mbalimbali za umeme.


Mhandisi Mathayo amesema mpaka kufikia leo saa sita mchana tayari walikuwa na wateja 61 ambao wameomba maombi mapya na kwa upande wa Manispaa ya Bukoba wateja 24 na kwamba mfumo huo wa Ni-konekt unawarahisishia wateja kupata huduma hata akiwa nyumbani bila hata kufika ofisini kama ilivyokuwa awali.


"Mfumo huo upo katika njia tatu njia ya kwanza ni kupitia kwenye Website kwa kuandika www.tanesco.co.tz au kupakua app ya Ni- Konekt na kwa wale wenye simu za kitochi (kiswaswadu) wanatakiwa kuandika *152*00# Kisha atajaza namba 4 halafu fuata maelekezo, Muhimu tu lazima uwe na namba au kitambulisho cha Nida" amesema Mhandisi Mathayo.


Ameongeza kuwa kupitia mfumo huo mpya wa Ni-konekt umeondoa malalamiko kwa mteja na wafanyakazi na kuondoa vishoka ambao walikuwa wakidanganya wateja na kwamba ule usumbufu wa kadi kupotea sasa hautakuwepo tena.


"Huu mfumo tuliozindua leo ni wa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera na niendeleee kuwapa moyo wateja wetu waendelee kutumia mfumo huu kwani ni salama kwao na kwetu pia",amesema.


Kwa upande wake Mteja wa kwanza wa Ni-konekt ambaye amehudhuria hafla hiyo fupi ya uzinduzi mpya Bi. Rosemary Peter amesema kuwa mfumo wa Ni-konekt umemrahisishia kupata huduma haraka na kuondokana na ule usumbufu wa njoo kesho na kwamba mfumo huo unapunguza na gharama/nauli kwa wale wanaotoka mbali.


Naye Mkandarasi Edwin Edward amesema kuwa mfumo huo umerahisisha sana kwao ambapo mfumo huo unatumia kompyuta na kujibiwa kwa haraka pale unapotuma data za mteja tofauti na awali ilikuwa ni kujaza fomu ambazo wakati mwingine zilikuwa zinapotea.


"Fomu ya mteja ilikuwa ikipotea lazima uiandike maana wewe ndiye uliyemfanyia kazi yake na pia lazima uweke lisiti ya malipo ambapo gharama hiyo ni yako, kwahiyo kwenye hila la mfumo huu mpya wa Ni-konekt mimi naona wameboresha sana", amesema Mkandarasi Edward.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post