Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE WATOA SOMO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU KUJIUNGA NA NSSF, WENYEWE WAHAMASIKA WACHANGAMKIA FURSA


Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mbeya, Mhe. Suma Fyandomo, akizungumza katika semina ya wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) ambapo aliwasihi kujiunga na kujiwekea akiba na NSSF.

Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mtwara, Mhe. Agnes Hokororo, akiwahimiza vijana kuelekeza fikra zao katika kujiajiri baada ya kuhitimu masomo kwa kuwa wamepata elimu ya kujiwekea akiba kutoka NSSF.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo akizungumza na wanafunzi wa Chuo IAA, ambapo aliwahimiza kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na NSSF.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Festo Fute, akizungumza wakati wa semina ya wanachuo wa IAA.
Meneja wa NSSF wa Sekta Isiyo Rasmi, Rehema Chuma, akitoa elimu ya Hifadhi ya Jamii na kuweka akiba kupitia mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa sekta isiyo rasmi kwa wanachuo wa IAA.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Josephat Komba, akizungumza wakati wa semina ya hifadhi ya jamii kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Wanachuo cha Uhasibu Arusha (IAA) wakiendelea na zoezi la kujaza fomu kwa ajili ya kujiunga na NSSF baada ya kupata elimu ya hifadhi ya jamii.
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Mwaitete Cairo akizungumza wakati wa semina na wanafunzi wa Chuo hicho
Mwakilishi wa TAHLISO, Katibu wa Rais TAHLISO Louisa Liheta akizungumza wakati wa semina hiyo.
Wanafunzi wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) wakisikiliza kwa makini mada kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba iliyotolewa na NSSF pamoja na baadhi ya wabunge.

**


Baadhi ya wabunge ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Katiba na Sheria wamewahamasisha wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kujiunga na kujiwekea akiba na NSSF kupitia Mpango wa Kitaifa wa Sekta Isiyo Rasmi chini ya kampeni ya “Boom Vibes na NSSF” iliyotua katika Mkoa wa Arusha.


Kampeni hiyo ya “Boom Vibes na NSSF” inalenga kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii pamoja na kuwahamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini na vyuo vya kati kuhusu umuhimu wa kujiunga na kujiwekea akiba na NSSF kwa ajili ya kuandaa maisha bora ya sasa na baadaye.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na wanachuo hao baadhi ya wabunge hao ambao ni Mhe. Suma Fyandomo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya. Mhe. Agness Hokororo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara na Mhe. Joseph Tadayo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga walisema kuna faida kubwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu kujiunga na kujiwekea akiba NSSF kwamba itawasaidia katika kutafuta mitaji mbalimbali ya kibiashara.


“Niwasihi sana fedha mnayopata kila mwezi iwe ni kutoka kwenye mkopo au kwa wazazi, msiitumie yote kwenye matumizi yenu, mnaweza kuanza kuweka akiba kupitia NSSF na mkianza kuweka akiba sasa basi itakapofika muda wa kumaliza elimu yenu, akiba mliyoweka inaweza kuwasaidia katika maisha yenu ya baadaye na hamtajutia uamuzi wenu,” alisema Mhe. Suma Fyandomo.


Kauli yake hiyo iliungwa mkono na Mhe. Joseph Tadayo: “Nilijiunga na NSSF na kuanza kuchangia kabla sijawa mbunge, miaka hiyo ya nyuma ya umri wangu huduma nyingi zilikuwa bure na hata ajira pia zilikuwa tele lakini kwa sasa hali haiko hivyo mtu anakuwa nacho sio kwa kile anachoingiza bali kile anachoweka, tunahitaji kuwa na utamaduni wa kuweka akiba tena kutokana na kile ulichovuna kutokana na jasho lako.”

Lakini Mhe. Agnes Hokororo alisema: “Vijana mnapaswa kuelekeza fikra zenu katika kujiajiri baada ya kuhitimu elimu yenu, ninyi mmepata bahati ya kuelimishwa kujiwekea akiba chini ya kampeni ya Boom Vibes na NSSF, changamkieni fursa hii kwani hamtajutia uamuzi wenu.”


Kampeni hiyo ambayo ni mkakati wa Mfuko wa NSSF wa kutembelea taasisi mbalimbali za elimu ya juu na kati nchini, ili kuhamasisha wanachuo kujenga tabia ya kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia kila mwezi ili hatimaye wanufaike na mpango wenyewe.


Akizungumza na wanafunzi hao, Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi, Rehema Chuma, alisema wanachuo ni wanufaika wakubwa wa mpango huo kutokana na kipato wanachokipata wanaweza kutenga ziada na kujiwekea akiba NSSF kwa manufaa ya sasa na baadaye.


Kuhusu namna ya kuchangia, Rehema alifafanua kuwa mwanachama wa NSSF anatakiwa kuhakikisha anachangia kiasi kisichopungua shilingi 20,000 kila mwezi au zaidi na kwamba anaweza kuchangia kidogokidogo kulingana na kipato chake ambapo hata akiwa na shilingi 1,000 kwa siku anaweza kujichangia.


Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Josephat Komba alisema lengo la Mfuko ni kuhakikisha inafikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wote waliopo katika sekta rasmi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wanafunzi wa elimu ya juu ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com