NYANI WAMVAMIA MAMA AKINYONYESHA NA KUMPOKONYA MTOTO MCHANGA ....WAMUUA

Mtoto mmoja Magharibi mwa Tanzania, amefariki dunia baada ya kuumia kichwa na shingo kwenye tukio la kushangaza la kuvamiwa na kundi la nyani wakati alipokuwa akinyonya nje ya nyumba yao.

Katika tukio hilo lililotokea juma lililopita (Juni 18), kundi la nyani kutoka hifadhi ya Gombe inayopakana na Kijiji cha Mwamgongo, wilayani Kigoma walimvamia, Shayima Said, mama na mkazi wa eneo hilo na kuondoka na mtoto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama alithibitisha kutokea kwa tukio hilo mnamo Juni 18,2022 na kueleza kuwa baada ya tukio hilo mwanamke huyo alipiga kelele kuomba msaada na ndipo majirani zake walipojitokeza kumdhibiti nyani aliyekuwa amebeba mtoto huyo.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya nyani huyo kuzidiwa, alimtupa mtoto huyo chini akiwa tayari amejeruhiwa kichwani na shingoni.

"Wananchi walifanikiwa kulikimbiza kundi hilo la nyani lililomvamia mwanamke huyo wakati akimnyonyesha wanaye, na kufanikiwa kumpata mtoto akiwa amejeruhiwa lakini baada ya kufikishwa katika kituo cha afya cha Mwamgongo alifariki dunia,"amesema Kamanda Manyama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post