Muonekano wa nyumba za watumishi hospitali ya rufaa kanda ya Chato
Na Daniel Limbe, Chato
SERIKALI wilayani Chato mkoani Geita imekabidhi nyumba 20 za makazi kwa watumishi 27 wa hospitali ya rufaa ya kanda ya Chato huku ikiwataka kuzitunza ili zidumu.
Mbali na hilo, imewataka wananchi wa kijiji cha Kitela kata ya Chato kuboresha mahusiano mema na watumishi hao, badala ya vitendo vya kishirikina vinavyoweza kusababisha kuzikimbia na kurejea kwenye makazi ya awali ambayo ni mbali na eneo la kutolea huduma.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Martha Mkupasi, amesema hayo leo wakati akikabidhi kwaajili ya kuanza kutumika nyumba 20 zilizojengwa na shirika la nyumba nchini (NHC) kwa thamani ya shilingi 1.1 bilioni ikiwa ni mkakati wa kuboresha makazi ya watumishi wa afya kwenye hospital hiyo.
"Mwenyekiti wa kijiji cha kitela nakuomba ufanye mikutano na wananchi ili uwaeleze umuhimu wa mahusiano na watumishi hawa...isije kutokea mtumishi anaanza kulalamika kwamba alilala akasikia amekabwa shingo, mara aliacha laptop (kompyuta mpakato) imezimwa na alipoamka kakuta imewashwa"amesema Mkupasi.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi huo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Brayan Mawala, amesema licha ya kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hizo, kiasi cha zaidi ya shilingi 1.7 bilioni zinahitajika ili kuboresha miundo mbinu ya madirisha, uzio, usawazishaji wa ardhi pamoja na matenki ya maji.
Kadhalika amedai mgao wa nyumba hizo kwa watumishi 27 kati ya wafanyakazi 114 umezingatia mahitaji muhimu ili kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa wagonjwa pindi kunapo hitajika kwa dharula.
Kwa upande wake mnufaika wa nyumba hizo, Dk. Matoke Muyenjwa, mbali na kupongeza hatua ya serikali amedai motisha ya nyumba hizo utasaidia kuinua ari ya utendaji kazi kwa watumishi hao, kuwa karibu zaidi na eneo la kutolea huduma kwa wagonjwa pamoja na kusaidia kuinua uchumi wa familia zao.
Kwa upande wake, Rose Masatu (mfamasia) amedai uwepo wa makazi hayo uewasaidia kupunguza gharama za maisha baada ya awali kulazimika kupanga mitaani ambako ni mbali na eneo la kazi, huku akiahidi kuendelea kuzitunza ili ziendelee kuwa kivutio kwa wengine.
Sambamba na hilo, ameiomba serikali kuendelea na ujenzi wa nyumba zingine kwa wafanyakazi ili kuwapungizia adha ya kuishi mbali na hospitali hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Martha Mkupasi, akipokelewa baada ya kuwasili kwenye mradi wa nyumba 20 za watumishi
Muonekano wa nyumba za watumishi hospitali ya rufaa kanda ya Chato