Maandalizi ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022
Utangulizi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo. Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012. Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.
Maana ya Sensa ya Watu na Makazi
Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. Takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022
Umuhimu wa kipekee wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na:-
Kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa;
Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali;
Taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote;
Kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi;
Taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira; na
Msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia. Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.
Madodoso ya Sensa
Sensa ya mwaka 2022 kama zilivyo sensa zilizopita itatumia aina mbili kuu za madodoso. Dodoso refu litakalotumika kuhoji asilimia 30 ya maeneo yote ya kuhesabia watu na Dodoso fupi litakalotumika kuhoji kwenye asilimia 70 ya maeneo yote ya kuhesabia watu.
Madodoso Mengine ni:-
Dodoso la Taasisi ambalo ni mahsusi kwa ajili ya wasafiri, waliolala mahotelini/nyumba za wageni, na waliolazwa hospitalini; na
Dodoso la Wasio na Makazi maalum ambalo ni mahsusi kwa watu wote wanaolala maeneo yasiyo rasmi, kwenye baraza za majengo mbalimbali, kwenye madaraja na maeneo mengine.
Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022
Utekelezaji wa sensa ya watu na makazi hufanyika katika awamu kuu tatu kuu ambazo ni Kipindi Kabla ya Kuhesabu Watu, Wakati wa Kuhesabu Watu na Kipindi Baada ya Kuhesabu Watu.
Kipindi Kabla ya Kuhesabu Watu
Kipindi kabla ya kuhesabu watu kinajumuisha Uandaaji wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa na nyaraka nyingine, Utengaji wa Maeneo ya Kuhesabia Watu na Uzalishaji wa Ramani, Uandaaji wa Nyenzo (Madodoso na Miongozo mbalimbali); Uhamasishaji, Sensa ya Majaribio ifikapo tarehe 29 Agosti 2021 ikiwa ni mwaka mmoja kamili kabla ya Sensa yenyewe; Kuunda kamati za sensa; kufanya mikutano na wadau wa takwimu; kufanya manunuzi, kufanya uchaguzi wa aina ya teknolojia itakayotumika, kuajiri wadadisi na wasimamizi, usambazaji wa vifaa; na kufanya maandalizi ya Tathmini ya Sensa.
Kipindi cha Kuhesabu Watu
Kipindi cha kuhesabu watu kinajumuisha kazi kuu na ya muhimu katika zoezi hili ya kuhesabu watu.
Kipindi Baada ya Kuhesabu Watu
Kipindi baada ya kuhesabu watu kinajumuisha Uchakataji wa Taarifa za Sensa, Uchambuzi, Utoaji wa Matokeo ya Awali, Usambazaji wa matokeo ya mwisho, uhamasishaji wa matumizi ya takwimu kwa watumishi wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.
Maandalizi ya sensa ya watu na makazi 2022 yalianza 2018, ikiwa ni kutenga maeneo ya kuhesabia watu, kutayarisha nyaraka muhimu za sensa kama vile madodoso, miongozo, fomu za kudhibiti ubora na kufanya sensa ya majaribio.
Kwa sasa maandalizi ya sensa yamefikia katika hatua zifuatazo;
Kuandaa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022;
Kutenga Maeneo katika wilaya 5 za mkoa wa Dodoma ambazo ni Bahi, Chamwino, Kondoa, na Chemba; na Wilaya moja ya Mkoa wa Singida (Singida Mjini);
Kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu inaendelea katika mkoa wa Singida katika wilaya za Manyoni, Ikungi; na mkoani Dodoma katika wilaya za Mpwapwa na Kongwa.
Kufanyika kwa ziara moja ya kimafunzo nchini Kenya kwa ufadhili wa UNFPA ambao wamefanya sensa ya kidigitali hivi karibuni na kujifunza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kufanya sensa kwa mafanikio. Matumizi ya teknolojia hii itasaidia kupunguza gharama za kufanya sensa na kupunguza muda wa kutoa matokeo ya sensa.
Kuandaa rasimu ya Dodoso la Sensa na nyaraka nyingine muhimu kama vile miongozo ya kufundishia, miongozo ya makarani wa sensa, miongozo ya wasimamizi wa sensa na miongozo ya waratibu wa sensa mkoa na wilaya.
Maswali Yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka 2022
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ina moduli kumi na nne ambazo zitatumika kukusanya taarifa za watu na makazi yao nchi nzima.
Maswali yatakayoulizwa yatahusu:-
Taarifa za kidemografia (umri, jinsi, uhusiano, hali ya ndoa, uraia, n.k.);
Maswali yanayohusu ulemavu;
Taarifa za Elimu;
Maswali ya uhamaji, pamoja na taarifa za Watanzania wanaoishi nje ya nchi
Maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa (vitambulisho vya NIDA, Mzanzibari mkazi, cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria, na leseni ya udereva)
Shughuli za kiuchumi
Umiliki wa ardhi na taarifa za TEHAMA
Taarifa za Uzazi na Vifo vilivyotokea ndani ya kaya
Vifo vitokanavyo na uzazi
Hali ya nyumba za kuishi na umiliki wa rasilimali mbalimbali
Maswali ya kilimo na mifugo
Mifuko ya hifadhi ya jamii.
Tofauti ya Sensa ya Mwaka 2022 na Sensa zilizopita:-
Katika sensa ya mwaka 2022 inatarajiwa kuwa na vitu vipya kama vile;
Kutenga maeneo ya kijiografia ya kuhesabia watu katika ngazi za kitongoji/mtaa na upatikanaji wa taarifa za kitakwimu katika ngazi za kitongoji/mtaa pamoja na kuwa na mipaka ya kudumu katika ngazi hizo;
Matumizi ya Vishikwambi (tablets) katika hatua zote za utekelezaji wa sensa kwa lengo la kupunguza gharama;
Nyongeza ya maswali yatakayowezesha upatikanaji wa taarifa zaidi za kitakwimu ikilinganishwa na Sensa ya Mwaka 2012:-
Taarifa za kidemografia (umri wakati wa ndoa ya kwanza);
Maswali yanayohusu ulemavu (Kichwa kikubwa, Mgongo wazi, Kifafa/Epilepsy, Mbalanga/storiasis na Usonji/autism);
Maswali ya uhamaji kulingana na mapendekezo ya IOM (International Organization of Migration);
Maswali kuhusu umiliki wa nyaraka za kitaifa (vitambulisho NIDA, vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wadogo, Mzanzibari mkazi, hati ya kusafiria, na leseni ya udereva);
Maboresho ya maswali ya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na idadi ya kaya ziliko kwenye sekta isiyo rasmi;
Umiliki wa ardhi na taarifa za TEHAMA
Takwimu za nyumba (orodha, hali ya umiliki na aina ya nyumba)
Maswali ya kilimo na mifugo
Hitimisho
Matarajio ya Ofisi ni kujipanga vizuri kwa kutumia rasilimali chache zilizopo ili kukamilisha kwa wakati shughuli zote za maandalizi ikiwamo:-
Kazi ya utengaji wa Maeneo ya Kuhesabia Watu katika ngazi ya kitongoji na mtaa ambayo ndiyo msingi wa kufanikisha sensa kwa ubora
Uandaaji wa nyaraka za sensa;
Uundaji wa vikosi kazi/units kwa lengo la kugawana majukumu; na
Ufanyaji wa Sensa ya majaribio tarehe 29 Agosti 2021