Joel Majok akiwa na mtoto wake
MWANAUME mmoja raia wa Sudan Kusini mwenye umri wa makamo ameibua gumzo mjini Eldoret baada ya kujiunga na shule moja ya msingi na mwanaye.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 32 aliyetambulika kama Joel Majok alianza darasa la tatu katika Shule ya Msingi ya Sosiani huko Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu.
Ripoti ya Citizen TV ilionyesha kuwa Majok, mkimbizi kutoka Sudan, alisema lengo lake kuu ni kujifunza lugha za msingi kwa sababu hajui kuzungumza Kingereza au Kiswahili.
“Nilianza shule kwa sababu ninataka maisha mazuri kwangu na kwa familia yangu,” Majok alisema. Mwanawe wa kiume Majok ambaye ana umri wa miaka nane pia ni mwanafunzi katika shule hiyo hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Sosiani Nicholas Kosgei aliguswa na kitendo hicho, akisema itasaidia pia kutia nidhamu miongoni mwa wanafunzi wengine ambao watamwona Majok kama mfano wa kuigwa.
“Alikataa ombi la kuanza katika darasa la saba kwa vile angependa kuelewa lugha za kimsingi,” Kosgei alisema.
Kulingana na Mwalimu Mkuu hatua ya kumpokea mzazi huyo shuleni humo itawatia moyo pia wanafunzi wengine kutia bidii katika masomo na kutokata tamaa maishani.