Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MJEMA AWATAKA WAFANYABIASHARA KULIPA KODI YA MAENDELEO KWA WAKATI


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akipatiwa zawadi na Afisa Mkuu Msimamizi wa kodi TRA Edwin Iwato.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa TRA nje ya ofisi yake.

Na Suzy Luhende, Malunde 1 Blog Shinyanga

MKUU wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amewataka wafanyabiashara wote wa mkoa wa Shinyanga wanaodaiwa kodi TRA, kulipa kodi kwa wakati ili kukamilisha mwaka wa fedha wa 2021/2022.


Hayo ameyasema wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Juni 3, 2022, ambapo amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawajalipa kodi mpaka sasa na wengine wanadaiwa madeni ya muda mrefu, hivyo wanatakiwa walipe kabla ya 20 Juni 2022 ili kuweza kufunga mahesabu ya mwaka.


"Nawaombeni sana wananchi wote ambao bado mnadaiwa kodi mlipe kwa wakati pia muwasilishe ritani ya VAT na mlipe kabla ya juni 20 mwaka huu ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya zuio SDL na PAYE kabla ya juni 7 mwaka 2022",amesema Mjema.


Pia Mjema amewaomba wananchi wote Agost 23 waweze kujitokeza kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, ili serikali isihangaike katika kupanga bajeti za kuwahudumia wananchi kama vile madawati zahanati na huduma zingine mbalimbali.


Kwa upande wake Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority - TRA) Edwin Iwato amesema wameanzisha kampeni ya Amsha Amsha Elimu kwa mlipa kodi mlango kwa mlango, ili kukamilisha mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa ajili ya kuwakumbusha wafanyabiashara ili waweze kulipa kwa wakati.


"Dira ya mapato ni kuongeza makusanyo ya ndani, kinachotakiwa walipe kodi kwa hiari kwani kufanya hivyo ni kujiletea maendeleo wenyewe na dhamira ya kampeni hii ni kufanya ulipaji wa kodi kuwa mwepesi"amesema Iwato.


"Tumeona tuanzishe kampeni hii ili kuwakumbusha wafanyabiashara kulipa kwa wakati na kumfanya mlipakodi kuwa mwepesi na kampeni hii tutapita mlango kwa mlango ili kuhakikisha kila mlipa kodi anaelimishwa kwa sababu suala la kodi ni la muhimu sana"amesema Iwato.


Aidha Iwato amewaomba wafanyabiashara wote wanapouza vitu lazima watoe risiti na wananchi wote wanaonunua wadai risti za EFD, kwani ukikamatwa umeuza bidhaa yako bila kutoa listi utatozwa Sh 3 milioni na ukikamatwa umenunua bidhaa bila kudai risti utatoa faini ya Sh. milioni 1.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com