Mbunge wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Anastazia Wambura akiwa katika picha ya pamoja na wabunge wanawake kutoka nchi za Afrika katika mkutano ulionza Juni 15,2022 jijini Arusha.
Na Rose Jackson,Arusha
Umoja wa wabunge wanawake wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na viongozi kutoka Afrika wamekutana jijini Arusha katika mkutano wa kimataifa wa wabunge wa kikanda ili kubadilishana uzoefu na mawazo haswa wa wabunge wanasiasa.
Akizungumza Juni 15,2022 katika ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu ulioandaliwa na bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Idea International na kufanyika Arusha Mwakilishi wa Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni mbunge wa bunge hilo Anastazia Wambura alisema ni vyema wanawake wakawa mstari mbele katika kuwania nafasi ya uongozi wa kisiasa kutokana na eneo ambalo maamuzi hufanyika.
Alisema wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kufikia ajenda ya usawa katika utoaji wa maamuzi kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa.
Wambura alibainisha baadhi ya changamoto zinazomkwamisha mwanamke kutowania nafasi ya uongozi ikiwemo majukumu ya kifamilia katika malezi pamoja na mila na desturi zinazowaonyesha kuwa wanawake ni duni.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa wabunge wanawake wa Bunge la Afrika mashariki, Fatuma Ndangiza alisema lengo la mkutano huo ni kuwapa kipaumbele wanawake viongozi kubadilisha uzoefu wa masuala ya uongozi haswa wale wanaoshiriki maswala ya ngazi za siaasa.
"Wabunge wataweza kujadili changamoto na Mafanikio ili waweze kusaidia wanawake vijana ili nao watambue kuwa Wana uwezo wa kufanya Siasa na kuwa na familia kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kubaini changamoy zinazowakumba wanawake wanasiasa", aliongeza Fatima.
Mmoja wa wadau wanaopigania haki za binadamu kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo,Agnes Sadiki alisema ni anashukuru kukutana na wanawake kutoka nchi mbalimbali kwani itasaidia kuhamasisha wanawake kuwania nafasi za uongozi mbalimbali na kuweza kufanya maamuzi.
Naibu Waziri anayeshughulika na Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Uganda, Dk.Rebecca Kadaga alisema mchango wa mwanamke katika kuleta maendeleo kwa jamii ni pamoja na kuzingatia usawa katika ngazi za maamuzi hivyo ni vyema wanawake wakapewa kipaumbele.