Jeshi la polisi Mkoa wa Njombe linafanya uchunguzi kuhusu tukio la vijana wanne kuvamia jengo la Watawa 'Masister' na kupora kiasi cha shilingi Milioni 2.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa amesema tukio hilo limetokea Mei 30 majira ya saa 12 jioni katika eneo la Emiliwa halmashauri ya Mji wa Njombe kituo cha Masister wa kanisa la Roman Katoliki katika jengo ambalo watawa wa kike wanalitumia kwa ajili ya wakala wa fedha.
“Vijana wanne walifika eneo la masister na mmojawao akawa anaongea nao kama vile anahitaji huduma akataja kiwango kikubwa na wale wakawa wanahesabu kama kipo ndipo akawaita wenzake wakaja na silaha aina ya bunduki wakachukua hela kiasi cha milioni mbili na kuanza kukimbia”, amesema Kamanda Issa
Amesema jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata vijana wawili kati yao walioshindwa mara baada ya kuanguka katika pikipiki na kuanza kushambuliwa na wananchi.
“Wakati wanakimbia kuna sehemu kumewekwa magogo walianguka,cha ajabu mmoja alibeba pikipiki na kuanza kukimbia nayo wakati hawa wengine wakabakia ndipo waliposhambuliwa na wananchi”, amesema Kamanda Issa.
Kamanda Issa amesema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini walipo vijana wengine huku akiwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kuhakikisha uhalifu unadhibitiwa.