ACCT YAANDAA KONGAMANO LA KUMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUTWAA TUZO YA HESHIMA YA BABACAR


Mwenyekiti wa ACCT Thobias Kyando akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuandaa kongamano la kumpongeza Rais Samia litakalofanyika kesho Jijini Dodoma na kueleza kuwa hatua hiyo itamuongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii.


************

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

CHAMA cha Wakandarasi Wazawa (ACCT) kimeandaa kongamano maalumu kwa ajili ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutwaa tuzo ya heshima ya Babacar ya mwaka 2022 nchini Ghana ambayo inatajwa kuitambulisha Tanzania kimataifa.

Hatua hii ni kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kupokea tuzo hiyo hivi karibuni kutoka kwa Makamu wa Rais wa Sekta Binafsi, Miundombinu na Viwanda kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Solomon Quaynor kwa niaba ya Rais wa Benki hiyo Dkt. Akinumwi Adesina kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa AfDB, Accra nchini Ghana tarehe 25 Mei, 2022.

Hayo yamebainishwa leo jijini hapa na Mwenyekiti wa ACCT Thobias Kyando wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuandaa kongamano Hilo linalofanyika leo kwa ajili ya kumpongeza Rais Samia na kueleza kuwa serikali imepata mafanikio katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kutokana na juhudi za wakandarasi.

"Rais Samia alistahili kabisa kupewa tuzo hii ya heshima kwa sababu amefanya mambo makubwa katika sekta ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, na bandari ndio maana akaibuka kidedea wa tuzo hiyo na sisi tukiwa wadau wa miundombinu tunampongeza sana,"amesema

Amesema wamechukua jukumu hilo kutokana na tuzo hiyo kuitangaza Tanzania kwa upande wa mafanikio ya ujenzi wa miundombinu unaowagusa moja kwa moja na kwamba kumekuwa na faida hasa kwa wandarasi wazawa kwasababu wao ndio wasimamizi wa maboresha ya miradi pindi wakandarasi wageni wanapoondoka.

Kyando ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapatia tenda mbalimbali ili waendelee kupata uzoefu hiyo itasaidia kuipunguzia serikali gharama ambazo imekuwa ikitumia kutoa tenda kwa kampuni za nje ya nchi.

"Ni vyema wakandarasi wazawa wakawa wanahusika moja kwa moja katika kutekeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchi hiyo itasaidia serikali kutumia fedha kidogo na kupata uzoefu kutoka kwa wakandarasi wa kigeni,"amesema.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa ACCT Profesa Mhandisi John Bura amesema kongamano hilo litafanyika katika ukumbi wa Jakaya kikwete Dodoma litakalo chochea ari kwa Rais Samia ya kufanya kazi kwa bidii na ubunifu mkubwa.

"Mgeni rasmi katika kongamano hilo ni Waziri wa ujenzi na uchukuzi Makame Mbarawa,tutatoa pongezi kubwa kwa Rais wetu kwa kupata tuzo kubwa ambayo inatupa nguvu kwa sababu hata sisi wakandarasi wazawa ameendelea kutujali kwa kutupatia kazi mbimbali za ujenzi tunachoomba tupewe fursa zaidi ili tuonyeshe uwezo zaidi kwasababu utaalamu unaweza ukanunuliwa kutoka nje kwa pale tutakapokwama,"amesema

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Ibra Contractors Lmt na Rais wa Sauti ya wanawake wajasiliamali Tanzania Maida Waziri amesema tuzo aliyoipata Rais Samia imewaheshimisha wanawake wakandarasi huku akiwataka wanawake wote kwa ujumla kuendelea kutambua na kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika sekta ya miundombinu.

Amesema kupitia tuzo hiyo Dunia imeweza kumtambua mwanamke mtanzania Katika picha nyingi ikiwemo nyanja za uchumi hivyo kama watanzania lazima kutambua umuhimu wa kile alichopewa Rais Samia na kutembe kifua mbele kwa sababu haikuwa kazi rahisi kuchukua tuzo hiyo.

"Tuzo hii haitolewi kiholela,Rais ameipata kutokana na ujenzi wa miundombinu na tuna haki ya kujivunia kwa sababu kama watanzania Rais Samia ameleta tuzo hiyo kubwa napenda kusema kuwa watanzania tunaona dira na muelekeo wa serikali ya awamu ya sita tunaona njia kubwa huko tunakoenda,"amesema

Maida amesema kigezo cha nchi kuonekana ni tajili mara nyingi hupimwa kwenye ujenzi wa miundombinu na kwa tuzo hiyo ambayo Rais Samia ameipata ameonyesha dunia kuwa Tanzania ni nchi yenye maendeleo kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post