Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ACVF YAZINDUA KAMPENI YA SEPESHA RUSHWA JIJINI DODOMA...MTAKA "TUSEPESHE KIUKWELI RUSHWA YA NGONO"


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akimkabidhi mmoja wa mabalozi wa ACVF cheti cha Mafunzo ya Siku Tano ya mapambano dhidi ya rushwa Jijini Dodoma
Baadhi ya Mabalozi wa Taasisi ya Sauti ya Wapinga Rushwa nchini (ACVF) wakifuatilia kwa makini Uzinduzi wa kampeni ya badili tabia sepesha rushwa yenye lengo la kuondoa kabisa vitendo vya rushwa kwa jamii.
Mlezi wa Taasiai ya Sauti ya wapinga rushwa nchini (ACVF) Abel Otieno akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni ya badili tabia sepesha rushwa Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA
TAASISI ya Sauti ya wapinga rushwa nchini (ACVF) imezindua kampeni ya badili tabia sepesha rushwa itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Arusha kwa lengo la kusaidia harakati za kuzuia vitendo vya rushwa.

Kampeni hiyo inahusisha mabalozi 365 ambao wamepatiwa mafunzo na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU).


Akiongea kwenye uzinduzi huo Jijini Dodoma Juni 26,2022,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ameitaka Taasisi hiyo kufanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa ili kukomesha vitendo vya rushwa.

Mtaka pia amewahakikishia mabalozi hao kuwa atakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanafanikisha kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano mkubwa wa wadau wote wapinga rushwa Mkoa Dodoma ili kuwachochea na kuongeza nguvu katika mapambano hayo.

"Nimefurahi mno kuona kuna watu bado hawalali wanaendeleza mapambano ya rushwa,nani asiyependa kuona rushwa inatokomezwa!niwaahidi kwa nafasi yangu nitafanya mkutano mkubwa na kuwashirikisha Klabu zote za wapinga rushwa wote wa shule ya msingi hadi vyuoni hii itasaidia kutengeneza mabalozi wa rushwa kwa kila maeneo ambao Serikali imepeleka fedha za miradi,"amesema


Amesema pamoja na juhudi hizo Serikali inataka kuona kunakuwa na mabalozi wapinga rushwa hadi vyuoni ambapo wanafunzi wengi wanalalamika kwamba mambo hayako sawa kutokana na rushwa ya ngono.


"Tunaposepesha rushwa lazima tuone umuhimu wa kuingia kiundani zaidi ili tusepeshe kiukweli, tusipoongeza juhudi hata watoto wetu wanaofanyiwa ukatili wa kingono mashuleni wakija kuajiriwa nao wanaweza kurithi vitendo hivyo na kuwafanyia wengine kama malipizi,niwahakikishie kwa hili mimi nitakuwa championi,"amesisitiza Mtaka


Mbali na hayo amesema kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na ACVF wataandaa mpango wa kutoa uhamasishaji wa elimu ya rushwa kwenye michezo ya umiseta na ngazi ya mikoa kutakuwa na mashindano ya michezo ili kila mmoja aone rushwa ni kitu kibaya.


"Tukifanya yote haya Jamii itakubali kuondoa mambo ya hovyo ikiwemo rushwa ya ngono lazima tuwawajibishe
,tusirithishe ujinga watoto wetu,aina hii ya ujinga haitajirudia kwa vizazi vijavyo na kama tuna watu badó wanawaza kurubuni watu kwa rushwa hiyo ni aina flani ya ujinga,"amesema


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Mabalozi wa Sauti ya wapinga rushwa (ACVF) Kubega Dominic amesema Kampeni ya Badili tabia,Sepesha Rushwa ilizinduliwa mnamo tarehe 01 Mei 2022, jijini Dar es Salaam Chini ya Afisa Wa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Bibie Msumi ikiwa ni mwendelezo wa Kampeni iliyozinduliwa Dodoma.


Amesema Kampeni hiyo inashika kasi na kufanya vema kwenye Mitandao ya kijamii kupitia kurasa za Facebook, Instagram,Twitter,Linked in, Google Business na YouTube na kwamba mara baada ya uzinduzi wa Kampeni hiyo wamefanikiwa kuandaa na kushiriki matukio mbalimbali Ngazi za Kanda .


"Tumeshiriki mdahalo wa Jumuiya ya Wapinga Rushwa uliofanyika tarehe 13 Mei 2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Chini ya Wanafunzi wa kitivo cha Falsafa na Maadili na Kongamano la Maazimisho ya Miaka 15 ya kuanzishwa Kwa Jumuiya za Wapinga Rushwa Vyuoni nchini Tanzania, lililofanyika tarehe 14 Mei 2022,"amesema


Amesema ACVF ikiwa ni Taasisi inayolenga kuongeza ufahamu juu ya rushwa ngazi ya kitaifa wataendelea kupaza sauti na harakati za kupambana na kuzuia rushwa nchini kwa kauli moja ya BADILI TABIA #SEPESHARUSHWA


"Kwa kubaini hayo ACVF tuliamua kusimama Vema na kuamini kuwa sababu kubwa inayopelekea kuendelea kushamiri vitendo vya rushwa ni tabia, na hilo ndilo chimbuko la kauli hii tunayotumia kuhamasisha jamii isemayo BADILI TABIA #SepeshaRushwa ili kutokomeza Rushwa lazima kubadili tabia,"amesema


Naye Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Victor Swella amesema Ofisi hiyo itashirikiana na ACVF kutoa elimu kwenye makundi mbalimbali na kuleta maana kwenye mapambano hayo.

Amesema lazima kuwe na mipango mizuri ya kuratibu namna ya kutoa elimu ili kuwafikia watu wote kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kuwafuata kwenye mitaa yao na minadani kufikisha ujumbe huu.


"Tupeleke zaidi elimu kwa watu wa chini
ambao wananyimwa haki yao Kwa sababu ya rushwa,Kuna wengine hata hawajui viashiria vya rushwa ni kazi yetu kuwaelimisha bila kuchoka ili kila mtu aishi kwa amani na utulivu ,"amesisitiza


Kwa upande wa mlezi wa ACVF Abel Otieno amesema kuwa katika kufanikisha uzinduzi wa Kampeni ya Sepesha Rushwa jijini Dodoma, Taasisi imefanikiwa kusajili Mabalozi wapatao 318 Maeneo mbalimabli nchini.


"Baada ya usajili, Mabalozi wapatao 200 walisajiwa kushiriki Mafunzo ya Siku Tano ambayo yalifanyika kuanzia Tarehe 13 hadi 17 Juni 2022 na kwamba kati yao ni Mabalozi 95 waliohitimu Kikamilifu mafunzo hayo chini ya Mwezeshaji Afisa wa dawati la Elimu kwa Umma Mkoa wa Takukuru Kinondoni Bibie Msumi,"amesema


Hata hivyo amesema dhamira ya Taasisi hiyo imekuwa ikikwamishwa na mambo mengi yaliyo juu ya uwezo wao ikiwemo uchumi mdogo ambao bado unategemea wadhamini katika kufanikisha matukio muhimu ya uelimishaji.


Amesema Mabalozi wengi hukumbwa na ugumu wa ratiba za masomo kwani wengi wao ni vijana wa Vyuoni na kushindwa kushiriki vema Matukio makubwa ya Taasisi na uhaba pia wa zana za uendeshaji wa Kampeni mitandaoni na hadharani na kukosa washirika wa kudumu ambao wataweza kuunganisha nguvu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com