Katibu Tawala, wilaya ya Tandahimba akizungumza na washiriki wa warsha ya vijana kuwa mabalozi wa Amani Wilayani Tandahimba.
Na Deogratius Temba
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amewataka vijana wa mikoa ya mipakani kutokubali kurubuniwa na kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjivu wa Amani au vurugu na watu wasio na nia njema katika taifa.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga warsha iliyoandaliwa na ya shirika la Global Peace Tanzania (GPF Tanzania), iliyofanyika katika wilaya hiyo yenye lengo la kujenga uwezo kwa vijana kutoka makundi mbalimbali ili wawe mabalozi wa Amani nchini.
“Vijana tunawaomba sana na kuwahimiza, msikubali kabisa mtu yeyote akuahidi zawadi au fedha au nafasi kwa sababu amegundua una changamoto flani, halafu ujihusishe kwenye vitendo vya uvunjifu wa Amani au vurugu, huyo mtu hakutakii mema, sio mtu mzuri, tuwakwepe kabisa watu wa aina hii” ,amesema Kanali Sawala katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu tawala Wilaya Juvenile Mwambi.
Kanali Sawala alisisitiza kwamba, serikali iko karibu na wadau wote ambao wanaendeleza jitihada za serikali za Kujenga uwezo kwa vijana ili wawe wazalendo na raia wema, sambamba na kuhakikisha elimu inayotolewa inayafikia makundi mengi zaidi ya vijana ili kutokomeza kabisa vitendo vya uvunjifu wa Amani katika ngazi zote.
Akitoa mada wakati wa warsha, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi wilayani Tandahimba, Danforde Mahundu, aliwataka Vijana kuwa mabalozi wa Amani, kwa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pale wanapoona makundi ya vijana yenye viashiria vya kuvunja Amani au kuleta vurugu.
“Vijana wengi mnaona watu wasio wazuri, wakizunguka mitaani, wengine wakijificha kwenye mgongo wa taasisi za dini, baadhi ya madereva wa bodaboda wanawabeba wanawasikia wanachoongea kuhusu uhalifu lakini hamsemi, Sisi Jeshi la polisi tupo tayari kushirikiana na wananchi katika masuala yote ya ulinzi na usalama muwe huru kutupa taarifa", alisema Mkaguzi Mahundu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Global Peace Foundation , Bi. Martha Nghambi alisema kwamba Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Kimataifa la kuzuia Ukatili (iDove), na utatekelezwa kwa kiindi cha mwaka mmoja ukiwa umelenga kuwafikia vijana wa makundi mbalkimbali wakiwemo viongozi wa dini, ambao watawezeshwa kujenga mijadala miongoni mwao namna ya kuboresha na kuimarisha zaidi amani katika wilaya za pembezoni ikiwemo Tandahimba, Mtwara.