UMOJA WA WAMILIKI NA WAENDESHA PIKIPIKI NA BAJAJI TANGA MJINI WAMPONGEZA RAIS SAMIA KUPUNGUZA BEI ZA MAFUTA "....AENDELEE KUUPIGA MWINGI"

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA),Mohamedi Chande
Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA) unampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua madhubuti anazochukua kuhakikisha kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwenye soko la dunia hazileti athari kubwa katika maisha ya wananchi na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Juni 5,2022 Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA),Mohamedi Chande amesema hatua madhubuti zilizochukuliwa na Rais Samia ni pamoja na kuweka ruzuku ya Shilingi Bilioni 100 ambayo wote tumeona jinsi ambavyo imesaidia kupunguza bei za petroli na dizeli nchi nzima kuanzia tarehe 1 Juni.

"Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ruzuku ya Shilingi bilioni 100 ya Rais Samia imesaidia kupunguza bei ya mafuta, ambapo kwa bandari ya Tanga, petroli imeshuka kwa shilingi 152 kwa lita na dizeli imeshuka kwa shilingi 476 kwa lita.Kabla ya ruzuku ya Rais Samia ya Shilingi Bilioni 100, sisi wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji mkoani Tanga tulikuwa tunanunua petroli kwa shilingi 3,137 kwa lita, lakini kwa sasa bei hiyo imeshuka hadi kufikia shilingi 2,985, huku kila lita moja ya petroli ikiwa na ruzuku ya shilingi 152",amesema Chande.


"Kwa upande wa dizeli, lita moja iliuzwa kwa shilingi 3,639 kwa lita kabla ya ruzuku ya Rais Samia, na sasa inauzwa kwa shilingi 3,162 kwa lita hapa Tanga ikiwa kila lita moja ya dizeli imewekewa ruzuku ya shilingi 476", ameongeza.

Amesema Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA) Mjini Tanga wanampongeza Rais Samia na serikali anayoiongoza kwa kuwajali wananchi na kuweka ruzuku hii kubwa kwenye bei za petroli na dizeli nchini.

"Tumeshuhudia jinsi ambavyo mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo baadhi ya nchi za jirani barani Afrika, yalivyokumbwa na tafrani kutokana na bei za mafuta kupanda duniani, huku kukiwa na uhaba na foleni kubwa kwenye vituo vya mafuta nchi hizo na hata vurugu sehemu nyingine.

Lakini hapa kwetu Tanzania kumekuwa na hali ya utulivu mkubwa kutokana na uongozi shupavu wa Rais Samia ambaye amehakikisha kuwa nchi inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha na pia kuweka ruzuku ambayo imesaidia kushusha bei ya petroli na dizeli nchini", amesema.

Amebainisha kuwa Ruzuku ya Rais Samia kwenye mafuta imeleta ahueni kwetu sisi wamiliki na waendesha pikipiki na bajaji, kwani imesaidia kupunguza ugumu wa maisha kwa kushusha gharama za uendeshaji wa pikipiki na Bajaji.

"Tunatoa wito kwa serikali ichukue hatua za kikodi kwenye Bajeti Kuu ya serikali itakayosomwa Bungeni mwezi huu, ili kupunguza zaidi bei za petroli na dizeli kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2022/23 unaoanza Julai 1,2022",amesema.

"Kupungua kwa bei ya mafuta kunaleta ahueni siyo kwetu sisi tu wamiliki na waendeshaji, bali hata kwa mamilioni ya Watanzania nchini wanaotumia huduma zetu ya usafiri wa pikipiki na bajaj katika shughuli zao za maisha kila siku",ameeleza Chande.


Amefafanua kuwa Pikipiki na bajaji hutumika kusafirisha abiria mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi, wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na pia kubeba mizigo, na hata wakati mwingine kubeba wagonjwa kuwapeleka hospitali ,hivyo ruzuku ya Rais Samia imesaidia sana kuleta ahueni kwa mamilioni ya Watanzania nchi nzima.

"Sisi Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Wilaya ya Tanga Mjini (UWAPIBATA) tunaunga mkono juhudi za Rais Samia za kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta na tunampongeza kwa uongozi wake mahiri na shupavu na kumtaka aendelee “kuupiga mwingi” katika jitihada zake za kuleta maendeleo nchini",amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post