Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UVCCM BAGAMOYO YAPULIZA KIPENGA UCHAGUZI NAFASI MBALIMBALI ZA UONGOZI

 


Katibu wa UVCCM Wilaya ya Bagamoyo Bw. Japhet Thobias

Na Elisante Kindulu, Bagamoyo


KATIBU wa umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Bagamoyo ,mkoa wa PWANI, Japhet Thobias, amewatangazia wanachama wote wa Chama hicho wenye sifa kuanza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika kata ndani ya Wilaya hiyo.


Katibu huyo wa UVCCM Wilaya aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa ofisini kwake mjini hapa mwishoni mwa wiki.


Bw. Thobias alisema fomu za Uongozi  ngazi ya kata zimeanza rasmi kutolewa tarehe 04/06/2022 na mwisho wake itakuwa tarehe 11/06/2022  kwenye Ofisi za CCM za kata kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa kumi jioni.


Katibu huyo wa UVCCM alizitaja nafasi  zinazogombewa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM kata, Katibu UVCCM kata, Wajumbe wa Baraza la Vijana kata (nafasi 5) na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kata.


Nafasi zingine ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Kata, Mjumbe kutoka Vijana kwenda Jumuiya ya Wazazi, Mjumbe kutoka Vijana kwenda Jumuiya ya UWT na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Vijana Mkoa kutoka kata. 


Katibu huyo alizitaja sifa za wagombea hao KUWA, awe na akili timamu, ajue kusoma na Kuandika, awe na miaka kuanzia 15 hadi 30 na awe mwanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM.


"Nawasihi Vijana wajitokeze kwa Wingi kugombea nafasi hizo za Uongozi ili kutumia fursa yao ya kidemokrasia katika Chama chetu," alisema Thobias.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com