****
NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE
TAASISI ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na halmashauri ya Chalinze, Mkoa wa Pwani wametoa huduma ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wenye matatizo hayo hivi karibuni.
Huduma hiyo iliyochukua siku mbili, ikiendeshwa na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Halmashauri ya Chalinze ilihudumia wananchi kutoka mkoa wa Pwani pamoja na mikoa jirani katika hospitali ya Msoga iliyopo Chalinze.
Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi hiyo Dkt.Peter Kisenge alieleza kuwa zoezi hilo limefanyika katika hospitali hiyo na idadi ya watu waliofika katika zoezi hilo kwa ajili ya upimaji, wapo waliopatikana na magonjwa hayo na wengine walikuwa salama.
“Tangu tumefika hapa mpaka leo tunamalizia zoezi hili la upimaji na tumeweza kupata idadi ya watu 422, ambapo kati ya hao asilimia 60 ya wagonjwa tumewaona wana matatizo ya shinikizo la damu kwa misuli yao ya moyo kutanuka na kutofanya kazi vizuri, na tumeweza kuwapeleka wagonjwa 20 katika Taasisis yetu kwa ajili ya kupata uchunguzi zaidi”.Alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliwashauri wananchi kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora na kuepuka vyakula vinavochangia unene wa kupitiliza kiasi, hususani vyakula vya wanga, nyama kwa wingi, unywaji wa pombe pamoja na uvutaji wa sigara uliiokithiri.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Dkt.Allen Mlekwa aliwapongeza wananchi wa Chalinze kwa kujitokeza kupata huduma ya vipimo vya moyo pamoja na mikakati ya Halmashauri ya Chalinze juu yakuendeleza vipimo hivyo.
Dkt. Mlekwa kwa niaba ya Halmashauri ya Chalinze aliishukuru Serikali ya awamu ya sita pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa ushirikiano wa kutoa huduma hizo.
Kwa niaba ya wananchi waliopatiwa vipimo hivyo, Bi.Gabriela Mtwale aliishukuru Halmashauri ya Chalinze kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa huduma walizozipata na kuomba zoezi hilo liwe linafanyika mara kwa mara ili kuokoa maisha ya nguvu kazi ya Taifa.