Mwanaume ambaye alijifanya kuwa afisa wa polisi kutoka makao makuu ya polisi Kenya amefikishwa mahakamani kwa makosa ya kumpiga na kumjeruhi afisa halisi wa polisi.
Edward Motaroki Nyaanga anatuhumiwa kumpiga Konstebo Dominic Obura akipiga doria mtaani Lang’ata na kumsababishia majeraha kichwani na mikononi.
Kwa mujibu wa karatasi ya mashtaka, Nyaanga alitekeleza hatia hiyo mnamo Alhamisi, Juni 16,2022 katika mtaa duni wa Southlands mtaani Lang’ata kaunti ya Nairobi.
Pia alikabiliwa na mashtaka ya kujifanya kuwa afisa wa polisi.
Mtuhumiwa anadaiwa kujifanya afisa wa polisi ili kumuingiza kibaridi Obura.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa mtuhumiwa ambaye alionekana kuwa mgeni alimwita konstebo Obura na kumwambia alikuwa afisa wa polisi kutoka makao makuu ya polisi.
Alipoambiwa kujitambulisha kwa kutoa kitambulisho chake cha kazi, aliingiwa na uhayawani na kumshambulia.
Afisa huyo wa polisi aliokolewa na wenzake ambao walimkamata Nyaanga na kumzuilia katika kituo cha polisi cha Lang’ata.
Alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera Ann Mwangi japo kupitia kwa waikili wake Mwihaki Ng’ang’a, Nyaanga aliomba mahakama kumhurumia.
Wakili Ng’ang’a alisema kuwa mtuhumiwa hana rekodi ya makosa na kwamba ni baba wa familia na mwananchi mtiifu.
Ng’ang’a alisema kuwa mtuhumiwa atazingatia masharti yote ya dhamana, mahakama hiyo ikimwachilia kwa dhamana ya shilingi 30,000 pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa tena Juni 28.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin