Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya habari-MAELEZO ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa (aliyesimama), akizungumza katika kikao Kazi baina ya WCF na Watendaji kutoka ofisi yake Ili kuwa na uelewa WA jumla kuhusu shughuli za Mfuko na maboresho ya hivi karibuni ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi. Kikao hicho kilifanyika Makao Makuu ya WCF, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi WCF Dkt. John Mduma (kushoto), akizungumza katika kikao Kazi baina ya Mfuko na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya habari-MAELEZO na watendaji kutoka ofisi hiyo. Kulia ni Msemaji Mkuu wa Serikali. Bw.Gerson Msigwa.
Baadhi ya Watendaji kutoka Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali
Baadhi ya Watendaji kutoka Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali
Baadhi ya Watendaji kutoka Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF Bw. Anselim Peter
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF Dkt Abdulsalaam Omar.
Baadhi ya Watendaji wa WCF
NA MWANDISHI WETU
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kutoa huduma bora kwa wafanyakazi wanaopata ajali wakiwa kazini.
“Tunashukuru kwa Mkurugenzi Mkuu na timu nzima ya WCF, kwa kuandaa kikao kazi muhimu kwani imekuwa nafasi muafaka ya kufuatilia taarifa kama maafisa habari katika utendaji kazi wetu wa kuisemea serikali, pia imetusaidia kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali kuhusu fidia kwa wafanyakazi” alisema Bw. Msigwa.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Bw. Msigwa amesema serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha WCF inakuwa imara kama Mfuko wenye jukumu la kufidia Wafanyakazi na tangu kuanzishwa kwake WCF imeendelea kutoa fidia kwa wafanyakazi wanaopata matatizo yanayotokana na kazi.
“Tumeweza kujua sheria iliyounda WCF na jinsi inavyofanya kazi, pia tunakazi kubwa ya kuelimisha jamii na watanzania juu ya nini wanatakiwa wakipate kutoka WCF” alifafanua Bw. Msigwa.
Katika kuboresha mazingira ya biashara na kuwezesha waajiri kuwasilisha michango kwa wakati, Serikali imeweza kupunguza kiwango cha michango kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.6 kwa Sekta Binafsi, lengo lingine likiwa kuwapa utulivu wafanyakazi endapo wakipata changamoto kutokana na kazi kwa kupata amani ya kulipwa fidia.
‘Nitoe wito kwa waajiri wote tulete michango kadiri inavyotakiwa. Tunajua wengi mnawasilisha lakini tuendelee ili tuweze kuwahudumia Wafanyakazi maana sio rahisi kujua ni wakati gani utapata madhara ukiwa kazini ama kupata maradhi ukiwa kazini. Mwajiri unapotoa michango ya Wafanyakazi wako inavyotakiwa unafanya mfanyakazi kufanya kazi akiwa na amani akijua inapotokea tatizo lolote basi WCF ipo kwa ajili yake na hiki ndio tungependa waajiri wote wakitekeleze.
Niwapongeze Waajiri wote mnaowasilisha michango yenu WCF, na ambao hamfanyi hivyo basi muwasilishe michango hiyo WCF kwa wakati.
“Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika kama sio duniani zenye Mfuko madhubuti wa Fidia kwa wafanyakazi ambao unafanya kazi vizuri ndio maana Shirika la Kazi Duniani -ILO limethibitisha kuwa WCF inaweza kutoa huduma zake mpaka 2048 hilo ni jambo kubwa sana kwa Wafanyakazi, wa kuwa na uhakika wana Mfuko imara wa kuwahudumia kwa muda mrefu” alisema Bw. Msigwa
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akizungumza wakati wa kikao kazi hicho alisema ni muhimu sana kwa waajiri kuwachangia watumishi wao ili waweze kupata fidia pindi wanapoumia wakiwa kazini.
Kikao kazi hicho kimekutanisha watendaji kutoka ofisi ya Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na watendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi – WCF.