Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo amesema anajiandaa kuyapeleka mahakamani makampuni ya simu nchini juu ya matumizi ya mabando ya data.
Kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, Shigongo ameandika: “Wakili wangu anajiandaa kuzipeleka kampuni za simu mahakamani, juu ya matumizi ya mabando na data; ukombozi umewadia.”
Kwa muda mrefu, watumiaji wa mitandao ya simu hususan wanaotumia simu janja, wamekuwa wakilalamikia kupandishwa bei kiholela kwa mabando ya huduma za intaneti kunakofanywa na makampuni ya simu bila kuwashirikisha watumiaji.
Malalamiko mengine ni kuhusu kuisha haraka kwa mabando hayo ambapo watumiaji wamekuwa wakilalamika kuwa wakati mwingine, mteja anaweza kununua bando la kiasi fulani cha fedha lakini likaisha ndani ya muda mfupi tofauti na matumizi ya kawaida.
Suala hilo limewahi kumuibua Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye kauli yake ya mwisho wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari, alieleza kwamba kama kuna mtu mwenye ushahidi wa kuibiwa bando na mtandao wa simu, basi atoe taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA kwa ajili ya hatua za kisheria.
Pia, kupitia akaunti yake ya Twitter, Nape amewahi kuandika: “Kumekuwa na manung’uniko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu nchini. Baada ya kutafakari kwa kina, nimewataka Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kuandaa taarifa ya kina ya hali halisi na hatua wanazochukua katika usimamizi wa mawasiliano ya simu nchini, na kuwaeleza watumiaji.
Kabla ya Nape kuteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo, mtangulizi wake ambaye alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewahi kuliagiza Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kushughulikia malalamiko ya wananchi na changamoto wanazozipata wakati wanatumia huduma na bidhaa za mawasiliano nchini, ikiwemo bei za mabando.
Hatua ya Shigongo kulipeleka suala hilo mahakamani kama alivyoeleza, huenda likazifanya kampuni za simu kuwajibishwa na kudhibitiwa katika suala la upandishaji holela wa bei za mabando na kupunjwa kwa wateja, jambo litakaloleta unafuu mkubwa kwa mamilioni ya watumiaji wa simu za mkononi nchini.