Chongolo alisema hayo mkoani Kigoma akiwa njiani kuelekea nchini Burundi ambapo atafanya ziara ya siku tatu nchini humo ambapo pamoja na mambo mengine atafungua uwanja wa michezo na kituo cha kukuza vipaji unojulikana kama Nkurunzinza Peace Park Complex uliopo mkoa Makamba nchini Burundi.
Katibu huyo Mkuu wa CCM alisema kuwa katika uchaguzi huu wa viongozi wa ndani ya CCM ni lazima wapiga kura wazingatie kuchagua viongozi wenye mapenzi ya kweli kwa chama ambao ndiyo msingi wa viongozi wa serikali kwa siku zijazo hivyo wakati huu ni muhimu kwa wapiga kura kutoa mwelekeo wa umakini wa chama hicho.
“Ni lazima kuzingatia uchaguzi wa viongozi ambao kwa dhamira zao wanaonekana kuwa na dhamira za kuwatumikia wananchi, mkikosea sasa mtakuwa mmekosea kwa miaka yote hivyo umakini katika uchaguzi wa kiongozi anayefaa ufanyike sasa na kwa umakini mkubwa,”alisema Chongolo.
Alisema kuwa wapo wagombea wenye hila ambao wanawania nafasi za uongozi ndani ya chama kwa dhamira zao binafsi na kwamba ni vizuri wapiga kura wakaliona jambo hilo na kuwaweka kando wagombea hao.
Katibu huyo Mkuu wa CCM anafanya ziara nchini Burundi kwa Mwaliko wa Chama cha CNDD – FDD ambapo safari yake itamfikisha hadi Bujumbura mji mkuu wa Burundi ambako atakutana na viongozi wa chama hicho na serikali ya Burundi.
Chongolo alisema kuwa anafanya ziara sasa nchini Burundi baada ya Katibu Mkuu mwenzake wa CNDD – FDD, Reverien Ndikuriyo kuwa ameshafanya ziara za kichama nchini Tanzania mara tatu.
Social Plugin