RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA SIKU TATU MKOANI KAGERA


Mkuu wa Mkoa Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza na vyombo vya habari leo Juni 5, 2022

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya siku tatu Mkoani Kagera kwa kuzindua Miradi pamoja na kuzungumza na wananchi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Juni 5, 2022 katika ukumbi wa ofisi za Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Mh. Rais anatarajia kuwasili Mkoani Kagera tarehe 8 Juni 2022, kwa kupitia Wilaya ya Biharamulo, Muleba, pamoja na Bukoba huku akisalimia wananchi katika Wilaya hizo.

Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa tarehe 9 Juni, 2022, Mhe. Rais atafanya ziara katika Wilaya ya Missenyi ambapo atazindua Mradi wa Maji Kyaka-Bunazi wenye thamani ya Shilingi Bilioni 15.7 na kutembelea pamoja na kukagua Miradi ya kiwanda cha Kagera Sukari ili kuhamasisha zaidi uwekezaji katika Mkoa wa Kagera.

Ameongeza kuwa tarehe 10 Juni 2022, Mh. Rais anatarajia kuzindua Msikiti wa JUMI' UL ISTIQAAMA BUKOBA uliopo Mtaa wa Tupendane Manispaa ya Bukoba pamoja na kuongea na wananchi wa Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba.

Mkuu huyo wa Mkoa Meja Jenerali Charles Mbuge amewaomba wananchi wote  kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote atakayopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ili kumpokea kwa shangwe, bashasha na nderemo.

Pia amewaomba wananchi wote kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa  kujitokeza kwa wingi sana kuanzia saa 12:00 asubuhi tarehe 10 Juni 2022, kuja kumsikiliza Mh. Rais Samia katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post