Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAGEUZI YA ELIMU KUZINGATIA UWEZO WA KUWAJENGEA WAHITIMU UJUZI WA KUTOSHA KUINGIA SOKO LA AJIRA


Na Mathias Canal, WEST-Dodoma

Katika mageuzi makubwa ya elimu yanayofanywa nchini serikali imekusudia kuzingatia kwa kiasi kikubwa kuwajengea ujuzi wa kutosha wahitimu ili kuwarahisishia kuweza kuingia katika soko la ajira ili waweze kuajiriwa au kujiajiri pasina kupoteza ubora wa elimu.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amyeyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe Didie Chassot ofisini kwake Jijini Dodoma Leo tarehe 1 Juni 2022.


Amesema kuwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili hususani katika maeneo ya kuongeza ujuzi kwa vijana na kuimarisha upatikanaji wa ajira pamoja na vyuo vya ufundi utaendelea ili kuhakikisha kuwa nchi hizo mbili zinaimarika na kuwa na weledi mkubwa katika sekta ya elimu.


Waziri Mkenda amesema kuwa endapo baadhi ya mapendekezo yatachukuliwa kwenye mijadala mbalimbali inayoendelea nchini ni pamoja na kuongeza nguvu na kuwekeza katika elimu ya ufundi na vyuo vya ujuzi wa aina mbalimbali.


Amesema kuwa miongoni mwa sekta ambayo Usiswi imejipambanua vizuri ni vyuo vya ukarimu na utalii hivyo serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kuboresha zaidi mahusiano ya vyuo hivyo katika nchi zote mbili.

Amesisitiza kuwa serikali inaangalia uwezekano mahususi wa kupeleka wakufunzi nchini Uswisi katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja ili kujifunza katika vyuo hivyo.

“Na nimewaalika kuleta wakufunzi wao hapa nchini ili kukaa kwenye vyuo vyetu waweze kutueleza wanachoona kama tunatoa huduma kwa ubora ule ambao unatakiwa”


Kadhalika, Waziri Mkenda amewaalika wawekezaji kutoka katika mataifa mbalimbali ambao wanaweza kuanzisha vyuo hapa nchini hususani vya utalii kwani milango ya uwekezaji ipo wazi.

Kwa upande wake Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe Didie Chassot amemuhakikishia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kuwa Uswisi itaendeleza ushirikiano katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kuimarisha ujuzi.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com