Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRUNDI AUAWA AKIJARIBU KUPORA KWA BUNDUKI AK 47


  Kamanda wa polisi mkoa Kigoma James Manyama akionyesha bunduki iliyokamatwa ambayo alikuwa nayo Raia wa Burundi aliyetaka kufanya tukio la uhalifu. (Picha na Fadhili Abdallah)

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma James Manyama (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kigoma.


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MTU mmoja anayeaminika kuwa raia wa Burundi ameuawa na wananchi kwa tuhuma za kujaribu kufanya tukio la uporaji kwa kutumia bunduki ambapo pamoja na kifo hicho bunduki moja aina ya AKA 47 imekamatwa.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, James Manyama akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma leo amesema kuwa mtu huyo ambaye jina lake halijafahamika hadi sasa alitaka kutenda tukio hilo jana jioni katika kijiji cha Kibuye wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Kamanda Manyama alisema kuwa awali kabla ya kutekeleza azima yake hiyo marehemu akiwa amejificha kwenye kichaka alikutana na mwananchi mmoja wa kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Yapemacho Kasiano ambaye alimuhoji marehemu sababu ya kujificha kichakani ambapo Marehemu alijibu kuwa alikuwa anatafuta njia ya kwenda Burundi.

Alieleza kuwa wakiwa kwenye majadiliano hayo ndipo Marehemu alitoa bunduki aliyokuwa ameficha kwenye koti lake na kumshambulia nayo mwananchi huyo ambapo hata hivyo risasi ilimkosa Mwananchi huyo na ndipo akamrukia Marehemu na kuanza kupigana akitaka kumnyang’anya Bunduki huku akipiga kelele.

Kufuatia kelele hizo wananchi walijitokeza kwa wingi na kuanza kumshambulia Marehemu kwa silaha mbalimbali za jadi ikiwemo mikuki na mapanga ambapo alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali baada ya kuvuja damu nyingi.

Katika tukio hilo Kamanda Manyama alisema kuwa pamoja na kifo cha marehemu pia polisi walikamata bunduki moja aina ya AK 47, risasi nne na ganda moja la risasi ambayo imetumika.

 Akitoa muendelezo wa taarifa ya watu waliokamatwa na viungo vya binadamu Juni 3 mwaka huu Kamanda Manyama alisema kuwa polisi wamefukua kaburi la mtu ambaye viungo hivyo vilifukuliwa na kuthibitisha kuwa vilikuwa ni viungo vya Bilihanyuma Suminda, mzee mwenye miaka 90 ambaye alizikwa mwezi Januari mwaka huu.

Kamanda huyo wa polisi aliwataja watuhumiwa hao akiwemo Bankana Zakayo (41) aliyekuwa Sengerema mkoa Mwanza ambaye alikuwa akipelekewa viungo hivyo na Miraji Nyambi (45) aliyekuwa dereva wa gari lililokamatwa na viungo hivyo ambao wote ni walimu wa shule ya sekondari Mwandiga wilaya ya Kigoma.

Sambamba na hao  aliwataja pia Mathayo Ndayishimiye (40) Mganga wa kienyeji kutoka nchini Burundi, Ramadhani Abrahaman (52) Mganga wa kienyeji, Adizino John (62), Nguno Manyanza (49), James Kibeba (68), Kelvin Fedha na Thobias Fundo (33).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com