Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TCB YAZISHUSHIA RUNGU AMCOS TATU CHATO


Na Daniel Limbe, Chato

KATIKA kile kinachoonekana ni kukunjua makucha, bodi ya pamba nchini (TCB) imevishushia rungu la adhabu ya shilingi 1,500,000 vyama vya msingi vya ushirika wa pamba(Amcos)  vitatu baada ya kukutwa na pamba chafu kinyume cha sheria.


Adhabu hiyo imezikumba Amcos tatu ikiwemo Nyakato, Munekezi na Buziku ambazo zimekutwa na makosa ya uchafuzi wa pamba, kuchanganya mchanga pamoja na maji kwa makusudi kwa lengo la kuongeza uzito na kujipatia fedha nyingi.


Mkaguzi ubora wa pamba wilaya ya Chato na Biharamulo mkoani Kagera, Samwel Mdidi, amesema vituo hivyo vya ununuzi wa pamba vilibainika kwa nyakati tofauti baada ya kusafirisha pamba chafu hadi viwandani licha ya kutambua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria.


Kutokana na hali hiyo, bodi ya pamba (TCB) imelazimika kuvipiga faini ya shilingi laki 5 kila kituo ili iwe fundisho kwa Amcos zingine zenye lengo la kukiuka sheria kwa maksudi.


Meneja wa kampuni ya ununuzi wa pamba ya NIDA iliyoko wilayani Kahama mkoani shinyanga, Edison Peter, amekiri kampuni yake kukamata pamba chafu iliyopelekwa kiwandani hapo na Amcos ya Munekezi pamoja na Nyakato.


Kwa upande wake, Meneja wa chama kikuu cha ushirika cha(CCU) Berino Msigwa,amethibitisha kukamatwa pamba chafu iliyokuwa imechanganywa na maji kutoka kwa amcos ya Nyakato, na kwamba mbali na adhabu iliyotolewa na bodi ya pamba, pamba hiyo ikipokelewa baada ya kuanikwa juani hadi kukauka.


Katibu wa Amcos ya Nyakato, Nkwabi Majalabala, amekiri kukamatwa na pamba iliyokuwa imechanganywa na mchanga huku akidai hali hiyo ilisababishwa na eneo dogo la ghara la kununulia pamba kutokuwa na ubora unaotakiwa.


Hata hivyo vituo vyote vitatu vimefanikiwa kulipa faini hiyo na kuruhusiwa kuendelea na ununuzi wa pamba katika msimu wa 2022/23.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com