Na Costantine Mathias, Bariadi.
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wamelitaka Jeshi la Polisi kudhibiti wizi na Unyang'anyi unaoendelea katika magari ya Abiria almaarufu michomoko siku za Jumanne na Alhamisi.
Wakizungumza leo kwenye Mkutano wa kujadili taarifa za robo ya tatu (mwezi Januari-March), uliofanyika Bariadi Sekondari, Madiwani hao wamesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiporwa pesa zao kwenye magari na watu wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo David Masanja amesema Unyang'anyi huo umekuwa ukifanyika siku za Jumanne na Alhamisi ambapo magari mengi hufika mjini Bariadi na Dutwa mnadani.
"Wananchi wa Old Maswa wanatekwa na wenye magari yanayokuja mnadani, wanakabwa, wanapigwa makofi na kunyang'anywa fedha zao...tunaomba Jeshi la Polisi kudhibiti hali hii" amesema Masanja.
Mwenyekiti huyo amelitaka Jeshi la Polisi kuweka mitego maalumu ili kuhakikisha wanakamata wahusika wa uhalifu huo, pia waangalie namna ya kudhibiti uhalifu wakati huu ambapo wananchi wanauza mazao yao ikiwemo pamba.
Naye Diwani wa Kata ya Nyangokolwa Charles Nkenyenge amesema kuwa katika kata yake pia kuna mwananchi amewahi kutekwa na watu wanaosafirisha abiria ambapo walimteka na kumnyang'anya fedha pamoja na kumtishia kumuua.
Diwani wa Kata ya Mhango Martine Singibala amesema tatizo la kutekwa wananchi limekithiri huku akilitaka Jeshi la Polisi kuongeza nguvu kufanya ukaguzi wa magari ya abiria.
"Mwananchi wangu alitekwa na wenye magari, gari lilitoka mjini lilielekea katani kwangu (Mhango), mwananchi akalisimamisha...baadae likageuza safari huku wakipiga mziki mkubwa na hawakusimamishwa na maaskari, yule mwananchi alinyang'anywa laki tatu na kutelekezwa njiani akarudi kutoa taarifa kwa Diwani" amesema Singibala.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo Kaimu Mkuu wa Kituo cha Polisi wilaya ya Bariadi Peter Ntinginya amewataka Madiwani kuwataarifu wananchi kutoa taarifa Kituo cha Polisi pindi wanakutana na masuala ya uhalifu na Unyang'anyi.
"Wilaya yetu ina Kata 31, hivyo Polisi ni wachache lakini tunajitahidi angalau Kila Kata kuwa na Polisi Kata mmoja, pia Kuna Kata zingine zinakaimiwa na Polisi mmoja....wananchi wanatekwa na kunyang'anywa watoe taarifa Kituo cha Polisi kwa hatua zaidi sababu magari hayo yamesajiliwa" amesema Ntinginya
Social Plugin