Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAHARIRI WA REDIO ZA JAMII WANOLEWA KUHUSU SENSA 2022


Na Mwandishi Wetu, Iringa

Wahariri wa Radio Jamii hapa nchini wameaswa kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha na kuwahamasiha wananchi ili waweze kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Said Ameir leo Juni 16, 2022 wakati wa ufunguzi wa siku ya kwanza ya mafunzo kwa wahariri wa Redio Jamii yanayofanyika mjini Iringa kwa siku mbili.


" Baada ya mkutano na Wamiliki wa Vyombo vya Habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, tumefanya mafunzo kwa Wahariri wa Mitandao ya Kijamii na sasa Wahariri wa Redio za Kijamii", alisisitiza Bw. Ameir.


Akieleleza zaidi amesema kuwa mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wadau ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uelimishaji na Uhamasishaji.


Aidha, amesema kuwa wahariri hao wanalo jukumu kubwa katika kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wote ili washiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi Agosti 23, 2022.


Kwa upande wake mmoja wa watoa mada kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hellen Hilary amesema Sensa ya Watu na Makazi itasaidia Serikali kupanga mipango ya Maendeleo kwa kuzingatia takwimu zitakazokusanywa.


Baadhi ya mada zitakazotolewa kwa Wahariri hao ili kuwajengea uwezo ni pamoja na; Sensa na Sheria ya Takwimu, Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi na Maandalizi yake, Sensa na Mbinu za Uripoti kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na Matumizi ya Mitandao ya Kijamii.


Sensa ya Watu na Makazi itafanyika Agosti 23, 2022 kote nchini ikilenga kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com