Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATETEZI WA HAKI WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUFUNGUA MLANGO WA MAJADILIANO KUHUSU UKWELI JUU YA MGOGORO WA LOLIONDO NA NGORONGORO.




Mratibu Kitaifa wa Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za Binadamu -THRDC Onesmo Ole Ngurumwa wakati wakizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la kutetea na kuinua maisha ya Wafugaji Tanzania Kamakia Robert akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka huu.

..............................

NA MUSSA KHALID

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania –THRDC umeipongeza serikali kwa kufungua mlango wa majadiliano kati ya asasi za kiraia na wizara ya katiba na sheria kwa lengo la kutafuta ukweli juu ya mgogoro wa Loliondo na Ngorongoro.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mratibu Kitaifa wa Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za Binadamu -THRDC Onesmo Ole Ngurumwa wakati wakizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu kikao cha wadau wa haki za binadamu ambacho kimefanyika Juni 22 mwaka huu kwa lengo la kujadili haki za binadamu na zoezi la uwekaji mipaka Loliondo sambamba na uhamaji wa hiari wakazi wa Ngorongoro.

Mratibu huyo ameipongeza serikali kwa jitihada za kuwaandalia mazingira rafiki wakazi wanaohama kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari huku wakiiomba kuendelea kuzingatia usalama pamoja na kutumia njia sahihi za ushawishi kwa wakazi hao.

‘THRDC inaamini kuwa njia bora ya utatuzi wa mgogoro wa Loliondo ni kuwa na majadiliano. Tunaishukuru Wizara ya Katiba na Sheria na Idara zote za Serikali zilizoshiriki katika kikao hicho muhimu kama mwanzo wa majadiliano ya kutafuta suluhu ya kudumu katika eneno la Loliondo na Ngorongoro bila ukiukwaji wa haki za binadamu.’amesema Olengurumwa

Mtandao huo pia umeishauri serikali kufanya tathmini na kupata idadi kamili ya wananchi waliokimbilia nchi Jirani kwa ajili ya matibabu ili angalau waweze kurudi nchini na wahakikishiwe kupatiwa matibabu hapa nchini.

Mtandao huo umewashauri viongozi na wananchi waliokamatwa na kushtakiwa waachiwe huru na washiriki katika mazungumzo ya maridhiano. Uchunguzi unaofanywa kuhusu kesi ya mauaji ya Askari wa Jeshi la Polisi ufanyike bila kuathiri watu wasiokua na hatia.

Kwa upande wao Mkurugenzi Mtendaji Shirika la kutetea na kuinua maisha ya Wafugaji Tanzania Kamakia Robert pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo Jumuishi Ngorongoro Loselia Maoi wameiomba serikali kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na mauaji ya askari wa jeshi la polisi aliyeuawa kwa mshale Juni 11 mwaka huu huku wakiishauri serikali kulipitia upya shauri la mauaji hayo linalowakabili viongozi kumi wa kijamii wanaodaiwa kuhusika mauaji hayo.

Wamependekeza viongozi na wananchi waepuke kuendelea kutoa kauli za kibaguzi na badala yake waendelee kujenga umoja na kuaminiana katika kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro.

Hata hivyo Watetezi hao wameishauri serikali kuweka mazingira rafiki ya utendaji kazi kwa vyombo vya habari nchini katika mgogoro wa eneo la hifadhi ya taifa ya Ngorongoro ili kuepusha kuchafua taswira ya nchi kwa mataifa mengine kutokana na vyombo vya nje kuripoti taarifa ya mgogoro huo kinyume na uhalisia hali wake

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com