TGNP YATOA MAFUNZO YA BAJETI YA MRENGO WA KIJINSIA KWA WADAU NA WABUNGE VINARA WA JINSIA BUNGENI DODOMA

Picha ya pamoja kati ya wawezeshaji wa TGNP Mtandao,wananchi na wabunge vinara wa jinsia  .

Mwenyekiti wa Chama cha wabunge wanawake na vinara wa jinsia Margaret Sitta akifafanua jambo kwenye mkutano wa wadau wa TGNP na kueleza  kuwa Wabunge vinara wa jinsia watahakikisha wanaisemea bajeti  ya mrengo wa Jinsia inafanikiwa na hatimaye makundi ya pembezoni kunufaika.

Mwezeshaji wa TGNP  Deogratius Temba alisisitiza jambo kwenye mkutano uliowashirisha wananchi na wabunge vinara wa Jinsia jana Bungeni Dodoma.




 
Na Dotto Kwilasa, DODOMA

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP,) umekutana na wadau pamoja na Wabunge wanawake vinara wa jinsia Bungeni Dodoma na kuwapa mafunzo ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia itakayowanufaisha wanawake na makundi yaliyoko pembezoni ili kuondoa mzigo unaowasumbua wanawake katika masuala ya afya,elimu,maji,haki ya uchumi ,kilimo na ukatili wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Juni 11,2022 Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka TGNP Deogratius Temba amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanaibua majadiliano chanya pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto za masuala mbalimbali ya kijinsia hasa kwa kundi la wanawake, watoto na kundi la wenye ulemavu.

Temba amesema TGNP imeendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika kujadili bajeti kila mwaka kwa mrengo wa kijinsia na kwamba lengo ni kuwa na maendeleo endelevu yenye kujumuisha ustawi wa makundi yote na kudumisha haki za msingi za binadamu.

"TNGP tunafanya kila jitihada zenye lengo la kuboresha sekta za huduma kwa jamii, sekta ambazo kwa kiwango kikubwa zinawagusa wanawake moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kuboresha miundo mbinu ya huduma za afya na elimu hii yote ni kuamsha ari kwa Serikali kutenga bajeti yenye kulenga na kuhamasisha utoaji wa bima za afya kwa gharama sawa na bure kwa wajane wenye uhitaji, wazee na wanawake na kaya masikini nchini,"amesisitiza.

Kutokana na hayo, Mwenyekiti wa Chama cha wabunge wanawake,Margaret Sitta amesema kwa kushirikiana na Wabunge wenzake vinara wa jinsia watahakikisha mara kwa mara wanaisemea bajeti hiyo ya mrengo wa kijinsia hali itakayoongeza uwekezaji katika kutoa elimu ya umuhimu na namna ya kuzuia magonjwa kwa watu wa pembezoni ili kupunguza gaharama za matibabu ya magonjwa yanayozuilika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uchumi shindani wa viwanda na kusisitiza kuwa maendeleo ya watu yanahitaji nguvu kazi ya afya bora.

"Tunawapongeza wenzetu wa TGNP kwa kutushirikisha sisi pamoja na akina mama hawa na walipokuja hapa niliwauliza kwamba je,wawakilishi wenu wabunge wanayajua haya, wamesema wanayajua kwa hiyo mimi nilikuwa nafikiri ni vizuri kushirikiana na wabunge wa maeneo yao kwa sababu taarifa ya majimbo tunapeana pengine taarifa wananchi hawana lakini wabunge wa majimbo wanajua nini kinafanyika katika maeneo yao," alisema.

Kwa upande wa sekta ya Maji,Mwenyekiti huyo wa wabunge wanawake Bungeni amesema watatumia nafasi yao kuishauri Serikali kutanua na kujazilisha mtandao wa huduma ya maji safi na salama ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo za maji kwa taasisi za umma kama shule na vituo vya huduma za afya.

"Ni jambo la kusikitisha kuona wanawake hawapati maji safi na salama,niwaombe wadau wote wa maendeleo kuendeleza sauti hii ya jamii lakini kwa kushirikiana na sisi wabunge ili kwa pamoja tuweze kuondokana na hii hali,tunatamani kuona hata vituo vya kulelea Watoto wenye changamoto na vituo vya wazee vinapewa maji bila gharama yoyote," alisema mama Sitta.

Naye mmoja wa wawakilishi wa mafunzo hayo na mdau wa masuala ya kijinsia kutoka Wilaya ya Kishapu,Mkoa wa Shinyanga Neema Maige alisema anatamani kuona majadiliano yaliyofanyika kwenye mafunzo hayo yanazaa matunda kwa kuwa amechoshwa na changamoto ya uhaba wa maji tikaka Wilaya yao.

Alisema ikiwa idara za maji za mikoa zitawezeshwa,hali ya upatikanaji wa maji kwa wajane, wazee, kwa tozo za viwango vya chini kabisa, au hata bila tozo yoyote itawezekana.

"TGNP imetuwezesha kukutana hapa na wabunge vinara wa Jinsia ,tuna imani watatusaidi kufikisha sauti ya jamii sehemu husika,tunatamani kilio chetu kisikike ili kuondokana na changamoto za barabara mfano wa barabara ya kilomita 35 kutoka njia panda ya Kolandoto mpaka halmashauri ya wilaya ya kishapu ni mbovu inachangia kupanda kwa nauli,bidhaa za vyakula pamoja na usafiri kuwa mgumu,"alisema.

"Wakati mwingine tunapishana na magari ya wagonjwa yamepasuka matairi na kusababisha ajali kutokana na ugumu wa barabara sasa vitu vya namna hii lazima Serikali ifike mahali iangalie namna ya kutusaidia ili na sisi wanawake wa pembezoni tufurahie matunda ya maendeleo,"alisisitiza.

Naye Venace Mbena ametumia nafasi hiyo kuishauri Serikali kupitia sekta ya Kilimo kuhakikisha inaweka mpango wa kufanikisha
 ushiriki wa wanawake na vijana katika uchumi shindanishi, huku akitoa mapendekezo kwa sekta ya kilimo kutenga rasilimali za kutosha kuwalenga wanawake na vijana katika ufikiaji wa mikopo ya masharti au riba nafuu.

"Ili kujikwamua kiuchumi nakuondokananna umasikini uliopo lazima kila mtu ashiriki katika mapambano ,kwa nafasi yangu natamani kuona upatikanaji wa teknolojia sahihi za uzalishaji na uhifadhi, na ufikiaji rahisi wa masoko wezeshi, ufikiaji sahihi wa taarifa za tafiti za mbegu bora na mifumo ya kilimo cha umwagiliaji,kujenga masoko mapya kwenye maeneo yenye mvuto mkubwa kwa bidhaa za wajasiriamali wanawake na vijana,"alisema Mbena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post