KAMATI YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO MA MAJI YAITAKA NAIC KUTOA ELIMU NA UHAMASISHAJI WA UHIMILISHAJI.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) akiwasalimu Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Mkoa wa Arusha mara baada ya kufika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni. Kulia kwake ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na kushoto kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mhandisi Richard Ruyango. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza kwenye kikao kifupi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru ambapo amewaeleza wajumbe hao kuwa Serikali imepanga kutoa mafunzo yatakayowasaidia wahitimu kwenda kujiajiri na sio kutegemea kuajiriwa. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (Mb) na kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Charles Mhina.


Wataalam kutoka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) wakitoa maelezo juu ya namna kituo hicho kinavyofanya kazi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea kituoni hapo kwa lengo la kuona namna kinavyofanya kazi.


Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na wataalam wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (hawapo pichani) wakati kamati hiyo ilipoingia kwenye maabara ya iliyopo hapo kituoni kwa lengo la kuona jinsi maabara hiyo inavyofanya kazi.


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kushoto) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakati kamati hiyo ilipotembelea Kumbi za Mihadhara zilizojengwa kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru.


Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kushoto) wakati kamati hiyo ilipotembelea maabara zilizopo kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Tengeru.

...................................


Kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo, mifugo na maji ameagiza kituo cha taifa Cha uhimilishaji (NAIC) kutoa elimu na uhamasishaji juu ya umuhimu na faida za kufanya uhimilishaji ili kuweza kupata mifugo na mazao ya mifugo bora.

Kamati hiyo imetoaaelekezo hayo Leo Juni 18 katika ziara yake ya kutembelea kituo hicho pamoja na wakala wa mafunzo ya mifugo (LITA ) kampas ya Tengeru ambapo walisema kuwa pamoja na kituo hiyo kuwa cha muda mrefu na kuwa na matawi katika Kanda mbalimbali bado mwamko wa wafugaji katika kufanya uhimishaji ni mdogo kutoka na kukosa elimu juu ya suala hilo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt Christin Ishengoma alisema kuwa alisema kuwa kama kamati wametembelea na wameona teknolojia ya hali ya juu na yenye manufaa kwa wafugaji iliyopo katika kituo hicho lakini changamoto iliyopo ni mwitikio mdogo wa wafugaji katika kutumia teknolojia hiyo.


“Tumeona kwanzia ukusanyaji wa mbegu na jinsi zinavyofanyiwa vipimo lakini pia tumeelezwa kila dume na aina ya mbegu yake ambapo sasa kinachotakiwa ni elimu na ushawishi kusudi waweze kuitikia jambo hili la uhimilishaji na kuweze kubadilisha na kuboresha mifugo yetu na kuboresha mazao yao,”alisema Dkt Ishengoma.

Mbunge wa Moshi vijiji Profesa Patrick Ndakidemi alisema kuwa hali ni mbaya kwa wafugaji katika majimbo yao hivyo kwa mbegu walizoziona katika kituo hicho ni vema wagani wakawafikia wafugaji na kuwapa elimu juu ya teknolojia hiyo ili waweze kuboresha mifugo yao.

“Kusema ukweli hali ni mbaya huko Kuna maeneo mengine ambayo hawataamini kuwa tuna kitu kikubwa hivi ambacho kinaweza kutoa huduma nchi nzima kwahiyo langu kubwa namuomba Mhe Waziri na timu yake ya wataalamu kuboresha shughuli za ugani juu ya uhimishaji ili iweze kuwafikia wafugaji huko waliko, tuweze kuboresha wale Ng'ombe wa kienyeji kwani bila ugani mambo hayataenda vizuri,” alisema Profesa Ndakidemi.

Kwa upande wake Naibu waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega alisema kuwa pamoja na kuwa na mifugo wengi nchini lakini Kuna wakati viwanda vinakosa usambazaji hivyo wizara kwa sasa Ina mpango wa wajasiriamali wa mifugo na uvuvi lakini pia wana kazi ya kwenda kuzungumza na wafugaji ili waipokee teknolojia hiyo.

“Lakini pia tutaviongezea vituo hivi nguvu ili kuweza kuboresha zaidi kwasababu vimechoka lakini pia kuendelea kufanya tafiti za kina ili kuweza kupata matokeo mazuri zaidi kulingana na aina ya Ng'ombe lengo likiwa ni kuboresha mifugo yetu hapa nchini lakini pia na vipato vya wafugaji,” Alisema Ulega.


Awali akisoma taarifa Kaimu mkurugenzi mtendaji wa kituo Cha taifa Cha uhimilishaji(NAIC) DKT Dafay Bura alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa huduma ya uhimishaji ni kusambaza mbegu bora zitakazoweza kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa ili kuinua pato la mfugaji na taifa kwa ujumla pamoja na kuimarisha lishe.

Dkt Bura alisema uhimilishaji huo unasaidia kuongeza uzalishaji wa Ng'ombe wa kisasa, kuinua kiwango cha Ng'ombe wa asili pamoja na kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza nje ya nchi mazao yatokanayo na mifugo kama vile nyama na maziwa.

“Uhimilishaji huu una faida nyingi mojawapo ni kuzuia kuenea kwa magonjwa ya vizazi,kuzuia gharama za kutunza madume, kuepukana na hatari za kujeruhiwa, kupata Ndama wengi kutoka kwa dume bora, kutumia mbegu za dume bora kwa muda mrefu hata kama amevunjika au amekwisha kufa pamoja na kuwa na wigo mpana wa aina ya mbegu unayohitaji,” Alisema Dkt Bura.

“Tuna jumla ya madume ya Ng'ombe 33 ambapo kutokana na takwimu za Ng'ombe nchini kuwa kubwa wizara kwa kushirikiana na kituo hiki tuanendelea na uhamasishaji wa shughuli za uhimilishaji kupitia programu maalum ya jambo ya uhimilishaji katika halmashauri mbalimbali na kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya Ng'ombe 3000 walihimishwa bure ikiwemo wilaya ya Ngorongoro, Pangani,Muweza, Lushoto na Mkinga lakini pia bado tunakabiliwa na changamoto ya mwitikio mdogo wa wafugaji hivyo tunahitaji kufanya kazi zaidi ili kukuza uelewa kuhusu manufaa ya uhimishaji,” Alisema.


Naye mtendaji mkuu wa wakala wa mafunzo ya mifugo (LITA) Dkt Pius Mwambele akisoma taarifa ya chuo alisema kuwa chuo kinawajibu wa chuo kuchangia upatikanaji wa wataalamu wa mifugo nchini kwani waliopo ni 3800 huku mahitaji yakiwa ni 17,400 lakini pia kuwezesha umahiti wa ujasiriamali kwa vijana ili waweze kujiajiri pamoja na kuongeza upatikanaji wa mbegu na bidhaa bora za mifugo kwaajili ya kuwahudumia jamii jamii ya watanzania.

“Mafanikio tuliyonayo ni pamoja na kuongezeka kwa udahili kutoka 798 mwaka 2012/2013 hadi kufikia 3,972 ya mwaka 2021/2022 pamoja na kuongezeka kwa mapato ya ndani kutoka bilioni 3 hadi bilioni 4.7 lakini pia tunakabiliwa na changamoto miundombinu mibovu ya madarasa na mabweni kutokana na uchakavu,” alisema Dkt Mwambele.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post