Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan akizungumza kwenye Mkutano wa Kupitia na Kuthibitisha Kanuni za Maadili ya Uandishi wa Habari Mtandaoni leo Jijini Mwanza.
***
BAADA ya kuutumikia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) kwa zaidi ya miaka 19 kama mkurugenzi mtendaji, Abubakar Karsan ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia taasisi hiyo ifikapo Desemba mwaka huu 2022.
Karsan ameitumikia taasisi hiyo kama Mkurugenzi mtendaji toka mwaka 2003, ambapo amesema kufikia mwezi Desemba 2022 atastaafu rasmi kuitumikia UTPC ambayo ameeleza imekuwa taasisi imara na kubwa nchini.
Akifungua mkutano wa kupitia kanuni za maadili ya vyombo vya habari mtandaoni jijini Mwanza leo, Karsan ametangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari na kubainisha kuwa, ameamua kwa hiari yeye mwenyewe kustaafu.
“Toka mwaka jana niliomba mimi mwenyewe kwenye bodi ya wakurugenzi nistaafu, nikapumzike na niweze kuwaachia vijana, lakini bodi ilikataa wakaniomba niendelee mwaka mmoja hadi mwaka 2022,” amesema Karsan.
“Niliwakubalia bodi na sasa ule mwaka mmoja utamalizika mwezi Desemba, mwaka huu, nami nakwenda kupumzika ili niwaachie wengine waweze kuendeleza taasisi hii,”ameeleza Karsan.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, UTPC tayari imefanya mchakato wa kumpata mkurugenzi mpya, ambapo amewaomba waandishi wa habari nchini kutoa ushirikiano mkubwa kwake.
“Mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya wa UTPC ulianza muda mrefu na tayari amepatikana, hivyo niwaombe waandishi wa habari nchini kutoa ushirikiano mkubwa kwake,” amesema Karsan.
Amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa UTPC wamepitia changamoto nyingi sana, ambazo zimefanya taasisi hiyo kusimama na kuwa imara zaidi.
Soma pia: