MABALOZI WA KODI WATEMBELEA MIRADI INAYOTEKELEZWA KWA KODI ZA WANANCHI


Mabalozi wa kodi wa hiari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mhe. Subira Mgalu pamoja na Mhe. Zulfa Mmaka wakitembelea ujenzi majengo ya Chuo cha Ufundi kinachojengwa jijini Dodoma wakati wa ziara ya kikazi kuonesha namna matumizi ya kodi za wananchi zinavyofanya kaziMuonekanao wa Soko Kuu la Wamachinga linaloendelea kujengwa jijini Dodoma ambalo pindi litakapokamilika litachukua wamachunga zaidi ya 3,000Mabalozi wa kodi wa hiari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mhe. Subira Mgalu pamoja na Mhe. Zulfa Mmaka (katikati) wakioneshwa ujenzi wa moja ya Majengo ya Mji wa Serikali (Magufuli City) uliopo Mtumba jijini Dodoma wakati wa ziara ya kikazi kuonesha namna matumizi ya kodi za wananchi zinavyofanya kazi.

***************
Na Mwandishi wetu
Dodoma.

WATANZANIA wameshauriwa kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia bajeti iliyopangwa ya Sh trilioni 41.48 kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Rai hiyo imetolewa na wabunge mabalozi wa kodi wakati wa ziara yao mkoani Dodoma ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa kodi za wananchi.
Miradi iliyotembelewa na mabalozi hao ni pamoja na ujenzi Soko la Machinga, Mji wa Serikali
'Magufuli City', Chuo cha Ufundi cha Dodoma na ujenzi wa Mzunguko wa Barabara.

Balozi wa Kodi Mhe. Subira Mgalu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, alisema kwamba, katika kuchochea maendeleo ya nchi ni vyema kuiunga mkono Serikali kwa kulipa kodi kwa hiari.

"Kwa Bajeti ya mwaka 2022/23, Serikali imepanga kukusanya shilingi trilioni 41.48 ambazo zinakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo ili kufikia lengo la kukusanya fedha hizo ni muhimu walipakodi na wananchi kwa ujumla wakalipa kodi kwa hiari na wakati,” alisema Balozi Subira.

Alisema kuwa, tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ameweka karibu sekta binafsi na kusisitiza kuwa pamoja na Serikali haifanyi biashara lakini imekuwa ikiandaa mazingira wezeshi ya ulipaji kodi kwa hiari.

Akizungumzia miradi aliyoitembelea balozi huyo, alisema thamani ya fedha imeonekana dhahiri na kusisitiza kuwa shughuli zitakazofanyika katika miradi hiyo zitakuwa na mwendelezo wa kuchangia pato la taifa na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

"Nitoe wito kwa wafanyabiasha wa kada mbalimbali wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na Watanzania wote tuendelee kulipa kodi kwa hiari, tuendelee kudai risiti kila tunapofanya manunuzi na wafanyabiashara watoe risiti kila wanapouza bidhaa zao.

Niwathibitishie Watanzania kwamba, endapo tutaendelea na uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari ikiwa ni zile zinazokusanywa na TRA na kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, nchi yetu itapiga hatua kubwa ya maendeleo", alieleza.

Balozi mwingine wa Kodi ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Zulfa Omary ambaye amesema kuwa, maendeleo ya nchi yoyote yanafikiwa kutokana na watu kulipa kodi.

"Ninawaomba watanzania msiwaogope TRA wanapokuja kuhamasisha ulipaji kodi kwasababu manufaa ya kodi yameonekana katika miradi yote ambayo tumeitembelea katika ziara yetu hivyo nawashauri na kuwasihi wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwasababu matokeo ya kodi mnazolipa yanaonekana wazi wazi," alisema Balozi Zulfa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo amesema kwamba, ziara hiyo ililenga kuonesha namna kodi zinazolipwa na wananchi zinavyotumika katika kuleta maendeleo.

“Mara nyingi tumekuwa tukiwahamasisha wananchi kulipa kodi lakini safari hii imebidi tuwapitishe mabalozi wa kodi kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa na kodi hizo ili watanzania nao waone kupitia vyombo vya habari jinsi kodi zao zinavyofanya kazi,” alifafanua Bw. Kayombo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post