Maafisa wa polisi eneo la Mikindu, Kaunti ya Meru wameanzisha uchunguzi baada ya afisa mkuu wa polisi kupatikana akiwa amefariki dunia katika nyumba ya mpenzi wake Jumamosi, Juni 25,2022.
Sajenti mkuu Moses Gakula anaripotiwa kunywa pombe na mwanamke huyo ambaye anafanya kazi katika saluni katika soko la Kiolo Ijumaa usiku kabla ya kupatikana amefariki kwenye kitanda chake.
Gakula alikuwa amevalia sare zake kamili za polisi huku akiwa na dawa mfukoni mwake.
Uchunguzi unaonyesha kuwa mpenzi wa afisa huyo alipokea simu kutoka kwa mwanamke mwingine ambaye inasemekana alikuwa na afisa huyo katika klabu moja na kumfahamisha amuendee akisema alihitaji matibabu.
Mpenzi wake marehemu anasemekana kumpa mwanamke huyo maelekezo ya mahali anapoishi lakini afisa huyo alikuwa tayari amefariki dunia wakati alipokuwa akipelekwa nyumbani kwa mpenziwe.
"Alikuwa mzima na alikuwa akinywa pombe na watu alipoanza kutokwa na jasho jingi kabla ya kupelekwa kwa nyumba ya rafiki yake. Alipatikana akiwa amekufa asubuhi iliyofuata," ripoti ya polisi ilisoma kwa sehemu.
Akithibitisha kisa hicho, OCPD wa Tigania ya Kati Chepkwony alisema kuwa Gakula amekuwa akikabiliwa na shinikizo la damu na alipewa uhamisho hadi kituo cha polisi cha Ankamia kilichokuwa karibu na nyumbani kwake.
Mwili wa marehemu umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Meru Level Five ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.
Chanzo - Tuko News
Social Plugin