RAIS SAMIA ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA KUCHAKATA NA KUSINDIKA GESI ASILIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini Mkataba wa Awali wa Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG Project) kwenye Hafla iliyofanyika tarehe 11 Juni 2022 Ikulu, Chamwino Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi na Wananchi kwenye Hafla ya utiaji saini Mkataba wa Awali wa Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG Project) iliyofanyika tarehe 11 Juni 2022 Ikulu, Chamwino Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Baadhi ya Wawekezaji mara baada ya Hafla ya utiaji saini Mkataba wa Awali wa Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG Project) iliyofanyika tarehe 11 Juni 2022 Ikulu, Chamwino Dodoma.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa awali wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia ambao uwekezaji wake ni Trilioni 70.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Rais Samia amesema mradi huo ni mkubwa na wa kimkakati licha ya kuwepo mingine ya kimkakati kama Ujenzi wa Reli ya Kisasa, Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere nchini. na kueleza kuwa kati ya fedha hizo asilimia 10 ya uwekezaji ni Trilioni 7ambazo zitatumika ndani ya nchi kwakuwa ni kiasi kikubwa kinajengwa ndani ya nchi.


Amesema mradi huo ni wa nchi nzima lakini mikoa unapotekelezwa Lindi na Mtwara ni lazima waone manufaa yake hivyo mazingira mahsusi yasisahaulike wakati wa majadiliano.


"Mchakato wa majadiliano na utekelezaji wa mradi ni lazima ujenge uwezo wa watanzania kwenye sekta hiyo dhamira ikiwa ni kwamba katika miaka ijayo vizazi vivune rasilimali za nchi na uwe na tija na manufaa ya kujitegemea,safari hiyo lazima ianze sasa hivyo ni lazima tuanze kujenga uwezo wa watanzania kushiriki kikamilifu na kutumia manufaa yatokanayo na mradi huu,”amesema Rais Samia.

Rais Samia pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa uwekezaji huo ni mkubwa wenye kuhususiaha utaalam na ujuzi wa hali ya juu, na kwamba biashara na uwekezaji wa hali ya juu namna hiyo unahitaji taasisi za udhibiti wa kodi, sheria, ulinzi kushiriki sababu unahitajika kulindwa.


"Wanaotakiwa kulinda ni sisi sio wawekezaji wakubwa kwa hiyo tujitayarishe kwenye maeneo hayo,niombe Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini(TPDC) kutambua kuwa wao ndio wabia kwa niaba ya nchi hivyo liwe la kimkakati na miaka ijayo wafanye shughuli hizo wao badala ya kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi,"amesema.


Sambamba na hayo Rais Samia ameitaka wizara ya Nishati kukaa na wizara ya Fedha na Mipango kuona ni kwa namna gani ushiriki wa TPDC kwenye mradi huo unakuwa wa tija na kwa manufaa makubwa zaidi.


“Nimelezwa kuwa maamuzi ya mwisho ya uwekezaji yanatarajiwa kufikiwa mwaka 2025 kwahiyo kusaini kwetu hapa haina maana tutaanza uwekezaji kesho bado tuna mengi ya kuzungumza,kuna vipengele kadhaa vimebaki vinahitaji mjadala kwahiyo tutegemee kwamba mjadala unaoendelea utafika pazuri na watamaliza mapema,''amefafanua

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post