SAGINI AMTAKA MKANDARASI KUMALIZA UJENZI WA JENGO HARAKA NA KWAMBA WIZARA HAIRIDHISHWI NA KASI YA UJENZI


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Uhamiaji Mtwara,tarehe 4 Juni 2022, ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Mtwara.Katika ziara hiyo ameambatana na Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji, Dkt Anna Makakala.


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini akizungumza kwenye kikao na Mkandarasi baada ya kukagua jengo la Idara ya Uhamiaji Mtwara.

............................................

Na Mwandishi wetu,

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amemuagiza mkandarasi wa ujenzi wa Jengo la Idara ya Uhamiaji mkoa wa Mtwara kukamilisha ujenzi huo ndani ya mwezi mmoja na kwamba Serikali haijaridhishwa na kasi ya ukamilishaji wa ujenzi huo.

Naibu Waziri Sagini amemuagiza Mkandarasi na Mshauri Mwelekezi wa mradi huo kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio siku ya Jumatatu tarehe 06 Juni wakiwa na mpango kazi wa kukamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi Juni 2022. Aliwakumbusha kuwa kazi ya umaliziaji inahitaji umakini mkubwa.

Aidha alisisitiza kwamba Wizara inahitaji watendaji wa idara ya Uhamiaji waanze kutumia jengo hilo mapema kwani kwa sasa wanatumia ofisi zilizotawanyika.

“Tabu yetu ni kasi ndogo ya Mkandarasi kukamilisha kazi ya ujenzi wa maeneo yaliyobakia. Kinachosikitisha ni kwamba wizara haijashindwa kumlipa Mkandarasi. Fedha zipo, lakini Mkandarasi yuko nyuma ya muda pamoja na kuongezewa muda zaidi.” alisema

"Nimeelekeza mkandarasi afike na mpango kazi Dodoma na kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili wakubaliane namna ya kukamilisha kazi kabla mwaka wa fedha 2021/2022 haujamalizika” alisema.

Naibu Waziri Sagini alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara Juni 4, 2022 baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Uhamiaji ikiwa ni moja ya ziara yake mkoani humo.

Aidha, Naibu Waziri Sagini ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kukubali kuwapatia ofisi baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wizara inaendelea kuwajengea ofisi.

Pia Naibu Waziri Sagini amevipongeza Vyombo vya Usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani vilivyopo mkoani Mtwara kwa utendaji kazi wao ukiondoa tukio moja lililolitia doa jeshi la polisi miezi kadhaa iliyopita. Alivitaka vyombo vyote kusimamia nidhamu ya askari, wakaguzi na maofisa wake ili matukio kama hayo yasijitokeze tena.

Aidha aliahidi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Uongozi wa Waziri Mhandisi Hamad Masauni itatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira na utendaji kazi wa vyombo hivyo.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala amesema Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Uhamiaji Mtwara umejengwa kwa kiwango kizuri lakini kasi yake hairidhishi kwani Idara ilitegemea ujenzi huo kukamilika Februari mwaka huu.

“Jengo limejengwa kwa kiwango kizuri lakini tunapima matokeo. Ukiangalia tupo kwenye asilimia 65 lakini tunahitaji ifikapo Agosti 2022 ujenzi uwe umekamilika” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post