Na Mwandishi Wetu, DODOMA
MBUNGE wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameshauri serikali ichukue maamuzi magumu wa kufufua viwanda 12 vya kubangua korosho kwa kuwa waliopewa wamegeuza kama maghala.
Akichangia leo makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2022/23, amesema ni wakati wa serikali kuchukua maamuzi magumu kwa kuwa wale wanunuzi waliovichukua hawana mpango wa kuvifufua na walipewa kwa bei ya ndogo.
“Walipewa kwa gharama isiyopungua Sh.Milioni 55, wamegeuza kama maghala sasa hivi, ni muda muafaka wa kufanya maamuzi magumu ya kurejesha viwanda hivyo serikalini na zipewe taasisi zetu kama Bodi ya Korosho, Halmashauri hata vyama vikuu vya ushirika ili ubanguaji wa korosho ufanyike,”amesema.
Amesema korosho iliyobanguliwa ina thamani kubwa kwenye soko la dunia na kutaka virejeshwe kwa kuwa walionavyo hawana mpango wa kufufua.
Katika hatua nyingine, Chikota ameipongeza serikali kwa kufanya mambo matatu kwenye sekta ya korosho ikiwamo kusambaza pembejeo bure kwa wakulima.
“Niipongeze kwa kuondoa ushuru wa forodha kwenye vifungashio vya korosho mwaka huu hatutakuwa na changamoto, nipongeze kitu kikubwa kilichofanyika cha kurejesha asilimia 50 ya export revy kwenda kwenye korosho, mtakumbuka mwaka 2017/18 hiki kitu kiliondolewa na mwaka huu kimerejeshwa,”amesema
Hata hivyo, ameshauri uwekezaji wa fedha nyingi kwenye Bodi ya Korosho ili kufikia lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayotaka ifikapo 2025 uzalishaji uwe umefikia tani 700,000.
Kuhusu wakaguzi wa ndani, Chikota ameshauri wapatikane watakaokuwa waadilifu, wazalendo na weledi wa kutosha ili ripoti za ukaguzi zisigeuzwe biashara kati yao na wakaguliwa.
Akizungumzia matumizi ya bandari, Mbunge huyo amesema bado matumizi ya bandari ya Tanga na Mtwara yapo nyuma licha ya kufanyika uwekezaji mkubwa.
“Nimpongeze Balozi wa Tanzania nchini Malawi, ndugu yangu Polepole wakati anawasilisha hati ya utambulisho amesisitiza kutumika kwa bandari ya Mtwara, naomba na mabalozi wengine wahakikishe bandari hizi zinatumika ipsavyo,”amesema.
Amemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufufua mazungumzo ya mradi wa gesi asilia huku akishauri muda ni huu wa kuwaelekeza wananchi wa Mtwara na Lindi kutumia fursa hiyo kubwa.
“Rais ametoa maelekezo maalum ya kutaka uwekezaji maalum kwenye mradi kwa maana ya upatikanaji wa huduma za kijamii, kutakuwa na wafanyakazi wa ajira rasmi na zisizo rasmi zaidi ya 10,000, haitakiwi Lindi na Mtwara ziwe kama ilivyo sasa, kuwe na maji ya kutosha, umeme wa uhakika na matibabu ili wageni wetu wapate huduma hiyo,”amesema.
Social Plugin