Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (IIA), CPA Zelia Njeza akizungumza.
Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (IIA), CPA Zelia Njeza akizungumza.
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA) imeipongeza Serikali ya Tanzania dhidi ya mabadiliko makubwa iliyopanga kuyafanya kupitia Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/23 ili kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Rais wa Taasisi ya Ukaguzi wa ndani, IIA, CPA Zelia Njeza amesema hatua hiyo ni kubwa kwa Serikali na inakwenda kuongeza ufanisi zaidi kwenye sekta ya ukaguzi wa ndani.
“…Kwanza tunaipongeza Serikali kwa kupeleka mapendekezo haya ya kutaka kufanya mabadiliko makubwa kwenye fani ya wakaguzi wa ndani, ambayo yanaanzia kufanywa kwa kukiboresha kitengo cha Mkaguzi Mkuu wa ndani, ‘Internal Auditor General (IAG)’,” alisema CPA, Njeza.
Aidha CPA, Njeza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya IIA alibainisha kuwa taasisi hiyo inaamini endapo mapendekezo hayo yatapitishwa umma utarajie ufanisi mkubwa kuongezeka na pia kuboresha utawala bora pamoja na kupungua vitendo vya ubadhirifu wa fedha.
“Wananchi wategemee kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji na utawa bora, hasa katika matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo eneo ambalo limekuwa na changamoto kidogo hapo awali.
Ametoa wito kwa wakaguzi wa ndani kujipanga katika utendaji ili kuiunga mkono Serikali dhidi ya mabadiliko makubwa ambayo imedhamiriya kuyafanya katika sekta hiyo.
Katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba (MB), akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23 bungeni Dodoma jana alibainisha kuwa, Serikali imepanga kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani kwa kuvijengea uwezo wa kitaaluma na kuongeza idadi ya watumishi katika fani mbalimbali kama vile TEHAMA, uhandisi, ukadiriaji majenzi, wakemia, wanasheria na fani nyingine ili kuondokana na dhana ya wakaguzi wa ndani kuwa na taaluma ya fedha pekee.
Waziri Dkt. Nchemba amesema, Serikali itafanya marekebisho ya Kanuni za Fedha za Umma kwa kuziwezesha Kamati za Ukaguzi kuwa na wajumbe wa nje watatu ikiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ili kuongeza uhuru na ufanisi wa kamati za ukaguzi kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2022.
Pamoja na mambo mengine, ameongeza kuwa Serikali itafanya marekebisho ya Kanuni zitakazo itazitaka Kamati za Ukaguzi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ndani kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kila robo mwaka, ikiwa ni pamoja na kutathmini muundo na majukumu ya Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ikiwemo kufanya stadi ya kujifunza kutoka nchi nyingine zenye Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu Serikali kama Tanzania ili kuangalia muundo unaostahili na kukidhi mahitaji ya Idara hiyo kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi.
"...Vilevile napendekeza Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kuwa na fungu lake (Independent Vote) pamoja na kuongeza idadi ya wakaguzi wa ndani ili kuimarisha na kuboresha ufanisi katika utendaji. Napendekeza kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 taarifa za wakaguzi wa ndani zipelekwe moja kwa moja kwa Internal Auditor General (IAG) kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya CAG," alisema Waziri Dkt. Nchemba katika hotuba yake bungeni mjini Dodoma.