Na Dotto Kwilasa , DODOMA.
SIKU ya baba imekuwa ni sherehe iliyobeba umaarufu duniani kwa ajili ya kuwaenzi na kuwaheshimu kina baba na kusherehekea ubaba, vifungo vya baba, na ushawishi wa baba katika jamii .
Siku hii ilipendekezwa na mwanamke mmoja anayejulikana kama Sonora Dodd wa Spokane, Washington nchini Marekani kama kutambua mchango wa malezi ya baba yake aitwaye William Jackson Smart ambaye alikuwa mwanajeshi wa zamani na aliwalea watoto sita akiwa kama mzazi pekee.
Hata hivyo ni ukweli usiopingika kwamba baba huyo (William)ni kielelezo cha wanaume wengi wanaoshikilia msimamo wao kwenye malezi ya watoto wao bila hata msaada wa Wanawake mfano ufuatiliaji wa karibu wa Afya na elimu kwa mtoto.
Nasema hivyo kwa sababu tumekuwa tukishuhudia wanawake wengi wakikosa utu na kuwafanyia ukatili watoto wao kwa kuwatelekeza na kwenda kuolewa na wanaume wengine huku watoto wao wakibaki chini ya uangalizi wa baba pekee.
Jambo hili limekuwa likileta ugumu kwenye jamii na kusababisha maumivu na sumu ya chuki kwa Watoto hivyo umuhimu wa baba unapaswa pia kutambulika na kuenziwa kila siku.
Kutokana na chimbuko la siku hii tunaweza kusema kwamba ni siku ya kuwaenzi kina baba wote wanaojitolea kutekeleza majukumu yao ya ubaba katika kuwalea watoto wao na kuwakumbusha wanaume waliojisahau kutimiza wajibu wao kuanza utekelezaji .
Kwa mara ya kwanza siku ya baba duniani ilifanyika huko nchini Marekani Mji wa Washington mnamo June 19, 1910 na siku hii huenda kwa kubadilika kila mwaka ambapo mwaka jana iliadhimishwa Juni 17 huku mwaka huu ikiwa inaadhimishwa Juni 19.
Siku hii Pamoja na mambo mengine mengi,yafaa kusherehekewa kwa namna tofauti kulingana na hali ya familia husika ambapo wanawake, watoto,marafiki na ndugu wengine wanapaswa kutoa zawadi kwa wanaume kama ishara ya kutambua mchango wao katika ujenzi wa jamii na kutengeneza familia bora Kwa kizazi chenye maadili mazuri.
Japokuwa wanawake wengi wa kitanzania wamezoea kupokea tu zawadi kutoka kwa wakina baba, yafaa kuitumia siku hii kuwanunulia zawadi kina baba ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha majukumu yaliyosahaulika.
Baadhi ya ni zawadi hizo ni pamoja na Waleti yenye rangi ya bluu iliyopoa kwa ajili ya kuhifadhi vitu kama pesa, vitambulisho na vitu vingine ambayo itaendana vyema na nguo anazopendelea,zawadi hii itategemea hali ya mnunuaji.
Nyingine ni Manukato, wababa wengu hupuuzia vitu ambavyo kwao wanaona havina faida yeyote, siku hii unaweza kumzawadia baba manukato yenye harufu nzuri kuonesha unajali muonekano wake na unadhifu wake kwani harufu nzuri huchangia kuonekana nadhifu.
Aidha ikiwa utapata nafasi ya kununua zawadi hiyo ya Manukato wa mpendwa wako,itakusaidia kutosahaulika kwa sababu hata asipoitumia na akakutana na mtu anayenukia kama yale Manukato atakukumbuka na kuwa na woga wa kukufanyia mabaya.
Zawadi nyingine ni Soksi,wanaume wengi ni wavivu kununua vitu vidogo vidogo kama soksi, leso, nguo za ndani kama vile vesti na n.k hivyo kwa kumnunulia soksi japo jozi tano ni namna moja wapo ya kuonesha unamjali katika siku hiyo muhimu.
Unaweza pia kununua Saa ya ngozi, na kumtunuku baba kama zawadi nzuri ambayo una uhakika ataifurahia ili kumuwezesha kutunza muda wake na kufanya mambo kwa wakati ili kulinda familia yake na kuitanguliza kabla ya nyingine.
Pamoja na hizo Kuna zawadi pia ya Mkanda wa kuvalia suruali zake pindi anapotoka kuelekea kazini.
Unaweza kuona hivyo ni vitu vidogo lakini vina maana kubwa sana hasa unapompa mtu kama zawadi, kuna vile vitu ambavyo unajua kama ni baba yako au mume huwa anavipenda ila anakosa muda wa kuvinunua au kuvifanya hii ndio siku ya kumfurahisha baba au mume katika siku yake hii muhimu.
Nimetimiza wajibu wangu kukukumbusha umuhimu wa kumjali baba,Usisahau kuwakumbusha na wengine umuhimu wa siku hii ..Nakutakia kheri ya siku ya baba Duniani.🙏🙏
Social Plugin