Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UTEKELEZAJI WA MRADI WA TIMIZA MALENGO KUDHIBITI VVU KWA VIJANA BALEHE


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene.

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kuhakikisha inafikia azma ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU)kwa asilimia 100 kwa vijana ili kuwapa nafasi ya kutimiza malengo yao.


Hayo yamebainishwa Jijini hapa wakati wa uzinduzi wa ugawaji na usambazaji wa vishikwambi kwa ajili ya kufundishia elimu ya VVU na ugonjwa wa Ukimwi, afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa timiza malengo kwa wasichana balehe na Wanawake vijana.


Simbachawene amesema, maendeleo ya nchi yanategemea nguvu kazi ya rasilimali watu na nguvu kazi hiyo kwa sehemu kubwa inafanya na vijana hivyo
utekelezaji wa mradi wa timiza malengo kwa wasichana balehe na Wanawake vijana utasaidia kwa kiasi kikubwa kunusuru kundi hilo kwenye maambukizi ya VVU.


"Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali kulinda kundi hili yapo masuala kadhaa ikiwemo maambukizi ya VVU na UKIMWI ambayo yamekuwa ni kikwazo kikubwa Kwa ustawi wa Vijana na Taifa kwa ujumla,ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa tishio la uchumi na maendeleo ya nchi na madhara yake yanaendelea kuwa ni changamoto katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa,"amesema.


Pamoja na hayo amesisitiza kuwa kama Taifa kuna kila sababu ya kuhakikisha kundi la vijana linalindwa ili kuimarisha nguvu kazi ya Taifa,kukuza uchumi,na kujenga Taifa lenye nguvu na kuongeza kuwa yapo mengi ambayo serikali inafanya kuhakikisha kundi hilo linawekewa mazingira wezeshi na salama yanayolinda ustawi wa akili na miili yao.


Ameeleza kuwa njia muhimu zitakazoweza kudhibiti maambukizi ya VVU Kwa vijana ni Kwa njia ya elimu kuhusu masuala ya UKIMWI ili kusaidia kundi hilo kutimiza malengo.


"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaridhishwa sana na namna mradi wa timiza malengo unavyotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa mradi huu ulianza katika mikoa mitatu na halmashauri 10 wamepanua wigo hadi kufikia mikoa mitano na halmashauri 18,"amesema.


Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko amesema mradi wa timiza malengo unagharimu fedha sh.bilion 55.2 na unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria (Global Fund) katika mikoa mitano.


Amefafanua kuwa mradi huo unatarajia kuwafikia wasichana belehe na wanawake vijana walioko nje na ndani ya mfumo wa shule wapatao million 1 lengo ikiwa ni kutoa elimu ya kutosha kuhusu maambukizi ya UKIMWI ili kukuza nguvu kazi ya Taifa.


"Msingi wa utekelezaji wa mradi huu ni kusaidia kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24 ili waweze kutimiza Malengo na ndoto zao pasipo kikwazo chochote,"amesema Maboko


Sambamba na hayo amefafanua kuwa mradi huo unalenga kusaidia wasichana walio ndani na nje ya mfumo wa shule kwa kuwajengea uwezo kifikra ,maarifa na maadili ili wakati wote wabaki salama dhidi ya maambukizi ya VVU na waweze kutumika na kulijenga Taifa.


Mmoja wa Mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Mtumba aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwajali vijana kwani wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ambazo zimepelekea wengine kukatisha ndoto zao.


"Elimu ya ukimwi ni muhimu kwetu kama vijana kwa sababu itatusaidia kujielewa,pia kwa wanafunzi ambao wapo katika umri wa kubalehe ambao mara nyingi huharibikiwa maisha kwa kujiunga na makundi yasiyoeleweka watanufaika ikiwa wataelimishwa kuhusu ukimwi bila kificho,"amesisitiza


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com