Na Karama Kenyunko Michuzi TV
VIGOGO wanne wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wakazi wa jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya USD milioni 1.8 sawa na Sh bilioni 4.2.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Timotheo Mmari leo Juni 30, 2022 imewataja washtakiwa hao kuwa ni Peter Gawile (58) Ofisa Rasilimali Watu wa TPA ,Casmily Lujegi (65), Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA, Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Hata hivyo, mshitakiwa Madeni Kipande ambaye alikuwa Mkurugenzi wa TPA, hakuwepo mahakamani kusomewa mashtaka kwani amefanyiwa upasuaji wa mgongo Muhimbili katika Kitengo cha Mifupa (MOI).
Imedaiwa, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhan Rugemalira, kuwa katika ya Oktoba Mosi,2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam washtakiwa walikula njama na kuisababishia TPA hasara.
Pia inadaiwa, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17,2015 washtakiwa wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani 1,857,908.04 .
Pia kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi,2020 huko TPA na maeneo mengine jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha Bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya Bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida kusikilizwa mahakama Kuu ama kupata kibali kutoka kwa DPP
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 14, 2022 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa
Kwa upande mwingine, Hakimu Rugemalira alihoji upande wa mashtaka sababu za kuwaleta washitakiwa mahakamani wakati upelelezi hujakamilika kwani ilishasemwa kuwa washtakiwa wanapaswa kufikishwa mahakamani upelelezi ukiwa umekamilika kwa lengo la kuanza kusikiliza.