*****************
Dar es Saalam. Katika kuendeleza utamaduni wa kujitoa kwa Jamii, Watumishi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wametoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wagonjwa wa Saratani waliolazwa Hospitali ya Ocean Road.
Vifaa vilivyotolewa kwa wagonjwa hao ni pamoja na miswaki, dawa za meno, mafuta ya kupaka, sabuni, khanga, madera, maji ya kunywa vitakavyo wasaidia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza baada ya kutembelea na kutoa msaada huo kwenye Hospitali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wawekezaji Bi. Anna Lyimo akimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa (TIC), alisema taasisi hiyo, huo utakuwa ni utaratibu wake kuendelea kushirikiana nao kwakuwa wanafahamu mahitaji yao.
“Tangu Juni 16, 2022 tulianza kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma na tumehitimisha leo Juni 24, 2022 kwa kuwatembelea wagonjwa wa saratani kuja kuwaona na kuwaletea msaada wa vifaa ambavyo vitakuwa vinawasaidia.
"Tumepokea wananchi pamoja na wadau wa uwekezaji zaidi ya 70 kwenye ofisi zetu na kuwapa elimu juu ya fursa za uwekezaji na tumehitimisha kwa kuja kutoa msaada kwa wagonjwa waliopo mahali hapa” alisema.
Matroni wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali hiyo, Chausiku Chapuchapu alishukuru baada ya kupokea msaada huo huku akieleza kuwa wapo wagonjwa waliolazwa ambao ndugu zao wako mbali hivyo utawasaidia.
“Wagonjwa wetu wanashukuru kwa misaada wanayopokea kutoka kwa taasisi na watu mbalimbali kwakuwa waliowengi ndugu zao wako mikoani ”, alisema Chapuchapu
Hata hivyo Watumishi wa TIC akiwemo Afisa Uerkezaji Bi. Veronica Mrema alisema wamepata faraja kusaidia wagonjwa wa saratani na wameahidi kurudi wakati mwingine.
Social Plugin