Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ametoa
maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na makampuni ya simu
kutatua kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano pamoja na
kuangalia namna ya kuwawezesha watanzania kuongeza matumizi ya simu janja
Maelekezo hayo ameyatoa leo Juni 1, jijini Dodoma wakati akipokea
taarifa ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali
zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania
“Kumekuwa na kero kwa wananchi kuingizwa kwenye huduma ambazo
hawakuziomba, TCRA na makampuni ya simu kaeni mtafute utatuzi walikomeshe hili mara
moja “, amesema Waziri Nape
Ameongeza kuwa, “Kila mtoa huduma ya mawasiliano aende kwa wateja wake
pamoja na wadau wanaowasaidia kutoa huduma kwa wananchi ili wasikilize malalamiko
na kuyatatua ,haiwezekani Serikali pekee ndio iwe inasikiliza na nyie makampuni
ya simu ina wajibu wa kufanya hivyo”.
Waziri Nape ameilekeza TCRA na makampuni ya simu kukaa na kutatua malalamiko
ya matumizi ya bando ambayo mtumiaji hajui limetumikaje ambapo ameelekeza makampuni
ya simu kuboresha program tumizi (mobile application) ili iwe rahisi kuisoma na
itoe taarifa nyingi zaidi ili kupunguza malalamiko ya watu kutojua wametumiaje
data zao
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaka TCRA na makampuni ya simu
kuona namna ya kumsaidia kila mtanzania kumiliki na kutumia simu janja kwa
kuangalia namna ya upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu na ikiwezekana
ufanyike utaratibu wa mwananchi kununua simu kwa mfumo wa kulipia kwa awamu ndani
ya mwaka mmoja au miwili ili kuongeza matumizi ya intaneti nchini
“Ikumbukwe kuwa Serikali iliondoa kodi kwenye simu janja lakini takwimu
zinaonesha matumizi ya simu janja yameongezeka kwa asilimia mbili tu, kwa
kuwezesha wananchi kutumia simu janja itaongeza watumiaji wa huduma ya
intaneti, makampuni mtapata fedha Serikali itaongeza mapato na mwananchi
atapata huduma anayostahili”, amezungumza Waziri huyo
Aidha, Waziri Nape ameipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuwa wa
kwanza kwenda kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyashauri makampuni
mengine kutekeleza hilo huku akiwashukuru wote waliowekeza katika sekta ya
mawasiliano na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na sekta
binafsi ili kumhudumia mtanzania
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose Vodacom
Tanzania ilifanya kazi kwa ushirikiano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)
na kujenga minara ya mawasiliano 23 ili kupanua wigo wa mtandao wa simu kufikia
asilimia 93 ya watu watanzania wanaopata huduma ya mawasiliano ya simu ikiwa
pia ni sehemu ya kampeni ya kampuni hiyo ya kuiunganisha Afrika ambayo
inatambua fursa za zinazotolewa na maunganisho ya kidijitali katika bara la
Afrika
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo ya simu ilifanya ukaguzi wa kina kwenye
huduma zao zote za kidijitali zinazotolewa na mawakala wasimamizi, na kugundua
baadhi ya changamoto ambazo zishughulikiwa na tayari simu za malalamiko kutoka
kwa wateja zimepungua kwa asilimia 30
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari
Social Plugin