WAZIRI NAPE AYATAKA MAKAMPUNI YA MAWASILINO KUACHA TABIA YA KUENDELEA KUTUMA UJUMBE AMBAO WATEJA HAWAJAOMBA







********

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametaka makampuni ya mawasiliano nchini kuacha mara moja tabia ya kuendelea kutuma ujumbe ambao wateja hawajaomba na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo ni kuwapotezea muda wateja wao.

Nape ametoa agizo hilo jana Jijini hapa wakati akipokea taarifa ya maboresho kutoka kwa timu ya mtandao wa Vodacom ambao walizunguka kwa baadhi ya mikoa kufanya uchuguzi wa malalamiko ya wateja ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri huyo kutaka kero za mitandao zitatuliwe haraka.

Amesema,kitendo hicho kimekuwa ni kero kwa wananchi kwani kinapoteza muda wa kutafakari jumbe hizo ambazo kuna wakati hazina faida kwa watumiaji husika wa mtandao na kusema kuwa hakipaswi kuendelea kuvumiliwa.

"Kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa wananchi ambao wanalalamikia suala la kuendelea kupokea jumbe mbalimbali ambazo hawakuziomba katika huduma na hivyo kugeuka kuwa ni kero badala ya huduma,naomba tuliangalie hili,"alisema.

Kutokana na hali hiyo,Waziri huyo wa Mawasiliano aliyataka makampuni yote yakae na watoa huduma kujadiliana kuhusu jambo hilo na kuona namna ya kuondoa tabia hiyo (ujumbe) kwa mtu ambaye hakuomba.

"Naagiza tabia hiyo ikome mara moja huu ni usumbufu kwa wateja,niseme wazi kuwa agizo hili halikulenga kampuni ya Vodacom pekee bali kwa watoa huduma za mawasiliano wote,"alisisitiza

Mbali na hayo alitoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kusimamia kwa nguvu zote agizo hilo ili kuondoa kero.

Amesema ni wakati kwa TCRA kwa kushirikiana na makampuni ya kutoa huduma waendelea kufanya maboresho hususani katika mfumo wa data na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa uelewa kwenye mitandao.

"Pamoja na changamoto hiyo ya kutumiwa meseji,TCRA wanatakiwa kukaa meza moja na makampuni ili kutafuta njia bora itakayowezesha Watanzania wengi kumiliki simu janja ikibidi hata kwa kukopesha na kulipa kidogo kidogo kwa kuwa Serikali inahitaji watu wengi kutumia mifumo ya data,"amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Sitho Mdlalose alisema kampuni yao ilipokea agizo la Waziri na kuamua kuzunguka katika baadhi ya mikoa kutafuta maoni ya wateja wao ambao walibaini kuna mambo mengi yanayofanyika na kuwa kero kwa watumiaji wa mtandao wano.

Ametaja baadhi ya mikoa waliyotembelea katika utafiti wao ni Mbeya,Mwanza, Arusha,Kilimanjaro na Dodoma .

"Tumezunguka mikoani na kukutana na wateja wetu wengi wakilalamika suala la bando kuisha hata kama mteja hakutumia lakini muda ukifika linaondolewa , jambo hili tayari tumelipatia ufumbuzi,"amesema Mkurugenzi huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post