Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI NDAKI AGAWA INJINI ZA BOTI KWA AJILI YA WAVUVI


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki,akizungumza kabla ya kukabidhi Injini tatu za Boti zenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 kwa wabunge wa majimbo ya Pangani, Mtwara Mjini na Iringa Vijijini ili ziweze kwenda kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao za uvuvi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za uvuvi, ambapo pia alisisitiza watumiaji wa injini hizo wazitumie kwa matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo. Hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi), Dkt. Nazael Madala akitoa maelezo kuhusu malengo ya sekta katika kuwawezesha wavuvi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuzungumza na kukabidhi injini tatu za boti zenye uwezo wa nguvu ya farasi 15. Hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso,akiipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kwa kuipatia Jimbo lake la Pangani Injini moja ya Boti yenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 kwa kuwa itakwenda kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao za uvuvi lakini pia katika kulinda rasilimali za uvuvi. Hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Sekta ya Uvuvi, Prof. Mohammed Sheikh akielezea uwezo wa Injini tatu za Boti ambazo zina uwezo wa nguvu ya farasi 15 wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo. Lakini pia alisema kuwa mpaka sasa Wizara imeshanunua jumla ya injini za boti 26,hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Mtenga (Mb) akiishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kwa kulipatia Jimbo lake la Mtwara Mjini Injini moja ya Boti yenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo, ambapo amesema hayo yote yamewezekana kutokana na kuwepo kwa uongozi sikivu na wenye mshikamano. Hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Mbunge wa Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) akiipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) kwa kuipatia Jimbo lake la Pangani Injini moja ya Boti yenye uwezo wa nguvu ya farasi 15 wakati wa hafla ya kukabidhi kwa kuwa itakwenda kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao za uvuvi lakini pia katika kulinda rasilimali za uvuvi. Hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi injini ya boti Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (kushoto) aliyeipokea kwa niaba ya wananchi wa Pangani wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo iliyofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi injini ya boti Mbunge wa Kalenga, Mhe. Jackson Kiswaga (kushoto) aliyeipokea kwa niaba ya wananchi wa Pangani wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo iliyofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akimkabidhi injini ya boti Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Mtenga (kushoto) aliyeipokea kwa niaba ya wananchi wa Pangani wakati wa hafla ya kukabidhi injini hizo iliyofanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma.


Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa nne kutoka kushoto), Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa tatu kutoka kulia) Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo ya Mtwara Mjini na Kalenga na Watendaji wa Sekta ya Uvuvi mara baada ya kukabishi injini tatu za boti zenye uwezo wa nguvu ya farasi 15. Hafla hii imefanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara zilizopo kwenye jengo la Benki ya NBC Jijini Dodoma.

..........................................

Na Alex Sonna-DODOMA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amekabidhi injini za boti kwa ajili ya wavuvi katika Halmashauri za Wilaya za Pangani, Mtwara Mjini na Iringa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi injini hizo leo Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara imeendelea na utaratibu wake wa kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia vifaa vinakavyowasaidia kuongeza uwezo wa kuvua mazao ya uvuvi kwa wingi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi hapa nchini.

“Injini za Boti tunazozikabidhi leo zina uwezo wa nguvu ya farasi 15 na tunazitoa kwenye Halmashauri za Wilaya za Pangani, Mtwara Mjini na Iringa ambapo kila Halmashauri itapata injini moja kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kuongeza uwezo wao wa kuvua lakini pia kulinda rasilimali za uvuvi,” alisema

Waziri Ndaki amewasihi wavuvi kuhakikisha wanavitunza vifaa wanavyopatiwa na Wizara pamoja na Wadau wengine wa uvuvi na kuhakikisha wanavitumia kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za uvuvi.

Aidha, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara imejipanga kununua injini nyingine 250 za boti katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kama kutakuwa na uwezakano zinaweza kuongezeka injini 70 zaidi ambapo kutakuwa na jumla ya injini 320.

Lengo ni kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya uvuvi unaongezeka na mchango wake katika kukuza kipato cha mvuvi na taifa kwa ujumla kinaongezeka. Kwa kufanya hivyo lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan litakuwa limetimia kwa kuhakikisha kipato cha wavuvi kinaongezeka na mchango wa uvuvi kwenye pato la taifa unaongezeka.

Vilevile Waziri Ndaki amesema kuwa injini hizo zitakazo nunuliwa zitatolewa kwenye vyama vya ushiriki vya wavuvi na hata kwa mvuvi mmoja mmoja mwenye uwezo kwa kuwa zitakuwa zikikopeshwa kwa riba ndogo sana ambayo haitawaumiza wavuvi.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Nazael Madala amesema kuwa Wizara imekuwa na utaratibu wa kuwawezesha wavuvi kwa kuwapatia vifaa mbalimbali vinavyowasaidia kuweza kuongeza uwezo wao wa kuvua mazao hayo kwa wingi zaidi.

Naye Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Pangani ameishukuru Wizara kwa kuwapatia injini hiyo na kwamba itakwenda kuwa msaada mkubwa kwa wavuvi katika shughuli zao za uvuvi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa rasilimaliza uvuvi. Lakini pia ameishukuru wizara kwa kuamua kujenga soko la samaki Pangani na kwamba wanapangani wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassan Mtenga licha ya kuishukuru Wizara kwa kuwakabidhi injini ya boti, ameiomba Wizara kuendelea kuwawezesha wavuvi kwenye vifaa vingine vya uvuvi ikiwemo majokofu ya kuhifadhia mazao ya uvuvi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com