*************
Na Dotto Kwilasa, DODOMA
WIZARA ya Afya imefanikiwa kuvuka lengo la kuwapatia chanjo ya polio watoto milioni 12.2 wenye umri chini ya miaka mitano.
Akizungumza na waandishi wa habari leo bungeni Dodoma Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto kwenye chini ya miaka mitano kwa awamu ya kwanza na ya pili umevuka lengo kuwa kuwachanja watoto milioni 12.2 badala ya watoto milioni 10.2 waliokuwa wamekusudiwa.
Amesema kuwa Kampeni hiyo ililenga kuwapatia chanjo watoto 10,295,316 kwa Tanzania bara.
"Nafurahi kutoa mrejesho kwa wananchi kuwa tumefanikiwa kuwapatia chanjo jumla ya watoto 12,131,049 (ambayo ni sawa na asilimia 117.8 ya malengo tuliyojiwekea).
"Ufanisi wa utoaji wa chanjo hii umetofautiana kutoka Mkoa mmoja hadi Mkoa mwingine kwa asilimia kama ifuatavyo.
"kwa ngazi ya Mikoa, Mkoa wa Ruvuma ulivuka lengo kwa asilimia 131, ikifuatia na Shinyanga kwa asilimia 128, mkoa wa Rukwa kwa asilimia 123, mkoa wa Pwani kwa asilimia 122, mkoa wa Arusha kwa asilimia 122.
" Mkoa mwingine ni Mbeya, Geita, Dar es Salaam na Simiyu yote ina asilimia 121, Mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora ina asilimia 118 , mikoa ya Kigoma, Njombe, Katavi ina asilimia 117, Mkoa wa Morogoro una asilimia 116, Mikoa ya Mara, Mtwara, Lindi na Tanga ina asilimia 115, huku mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza ina asilimia 114, na Mikoa ya Manyara na Iringa ina asilimia 113, wakati huo Mikoa ya Songwe na Kagera ikiwa na asilimia 111" ameeleza Ummy.
Akitoa mrejesho wa kampeini hiyo ya chanjo ya polio kwa watoto wa chini ya miaka mitano Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Polio hapa nchini.
Amesema kuwa Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu aliyeathirika kwenda kwa mwingine kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa na kinyesi chenye virusi vya Polio.
"Virusi vya Polio vinapoingia mwilini huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha madhara kiafya ikiwa ni pamoja na kupooza kwa ghafla kwa kiungo au viungo na hata kupelekea kifo.
"Dalili za awali za ugonjwa wa Polio ni pamoja na homa, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika, kukakamaa shingo na maumivu ya viungo.
"Ugonjwa wa Polio hauna tiba,njia kuu ya kuzuia ugonjwa huu ni kuwapatia chanjo ya polio watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano" ameeleza Ummy.
Ummy amesema kuwa mnamo tarehe 17 Februari 2022, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa taarifa ya kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa Polio (Wild polio Virus) nchini Malawi na mnamo mwezi Mei 2022 nchi ya Msumbiji ilitoa taarifa ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo nchini mwao.
Amesema kuwa Tanzania iliripoti uwepo wa ugonjwa huu mara ya mwisho mnamo mwaka 1996 toka Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi.
"Katika Bara la Afrika ugonjwa huu ulionekana mara ya mwisho nchini Nigeria mwaka 2016, na hivyo mnamo Agosti, 2020 Afrika ilitangazwa kutokomeza ugonjwa huu na kamati ya Kimataifa ya kutomeza ugonjwa wa polio.
"Kufuatia kuonekana kwa ugonjwa huu katika Ukanda ya kusini mwa Afrika, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa tamko kuwa Polio ni janga la Kimataifa.
"Janga hili linapeleka nchi zote zilizo katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika yaani Tanzania, Malawi, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi kutokana na kuwa na mwingiliano wa kijamii baina ya nchi hizi" ameeleza Ummy.
Social Plugin