Idadi ya waliofariki dunia katika ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la Modern Coast nchini Kenya imefikia 33.
Hii ni baada ya miili zaidi kuopolewa kutoka kwa mabaki ya basi hilo katika shughuli ya uokoaji mnamo Jumatatu, Julai 25,2022.
Kamishna wa Kaunti ya Tharaka Nithi Nobert Komora alithibitisha kuwa watu 10 walinusurika kwenye ajali hiyo mbaya lakini walilazwa katika hospitali mbalimbali wakiwa katika hali mahututi huku shughuli ya kutafuta miili zaidi inayoaminika kuzama mtoni inaendelea.
Katika mkasa huo wa Jumapili, Julai 25, 2022 basi hilo lilipoteza mwelekeo na kutumbukia mita 40 ndani ya mto Nithi katika kaunti ya Tharaka Nithi nchini Kenya.
Katika taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wake wa kijamii, kampuni ya mabasi ya Modern Coast ilisema gari hilo la kubeba abiri 45, na nambari ya usajili KCF 614 U, lilikuwa likielekea Mombasa kutokea Meru.
"Bado tunaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo. Jumla ya waliofariki wanahofiwa kuongezeka huku shughuli za uokoaji zikiendelea kuwakomboa waliokuwa wamekwama chini ya mabaki na mtoni," ilisoma taarifa hiyo kwa sehemu.
Kampuni hiyo iliomboleza pamoja na familia na wapendwa wa walioangamia na pia kuwatakia nafuu ya haraka wanaouguza majeraha.
Makosa ya devera yaliyosababisha ajali
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Tharaka Nithi Donatha Chali amesema dereva wa basi hilo alijongea daraja hilo kwa kasi ya juu na kupuuza ishara za barabarani ambazo zinawalekeza madereva kupunguza mwendo kasi.
Kwa mujibu wa Chali, daraja hilo ni eneo hatari na limeshuhudia ajali nyingi ambazo zimegharimu maisha ya watu wengi.
Basi hilo huenda lilikumbwa na shida ya breki kufeli
Ripoti za awali zilielezea kuwa basi hilo huenda lilikumbwa na shida ya kufeli kwa breki, kuanguka mtoni na kuzama mita 40.
Kauli za walioshudia ajali hiyo zilioana na ile ya polisi, wakisema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi na liligonga kingo za daraja hilo kabla ya kuanguka mtoni.
“Basi hilo lazima lilikumbwa na tatizo la breki kugoma kwa kuwa lilikuwa kwa kasi ya juu ajali hiyo ilipotokea,” Nicholas Mutegi, mmoja wa walioshuhudia ajali hiyo, amenukuliwa na Nation.
Mke wa dereva wa basi la Modern Coast lililotumbukia kwenye daraja la Tharaka Nithi Jumapili na kuua zaidi ya 30, amefichua nyakati zake za mwisho akiwa na familia hiyo.
Akihojiwa na wanahabari Jumatatu, Mama Mercy alisema mara ya mwisho alizungumza na mumewe, Mzee Simba, mwishoni mwa wiki alipokuwa akimtembelea binti yao anayesoma shule ya bweni.
"Nilikuwa nimehudhuria mkutano wa mzazi katika shule ya binti yetu na alizungumza naye na kuahidi kumtumia pesa na tangu wakati huo hatukuzungumza tena. Simu yake ilikuwa haipatikani,” alisema.
“Baadaye jioni, nilipigiwa simu na watu wakiniuliza kama ni kweli basi huko Meru lilipata ajali na Mzee Simba ndani yake… Lakini sikuweza kuthibitisha hadi nilipotazama habari za saa tisa",alisema.
Alikuwa akizungumza nje ya afisi za kampuni ya basi alikokuwa ameenda kuthibitisha kwamba mume wake ndiye aliyekuwa nyuma ya usukani wa basi hilo lililoharibika.
Mama Mercy alisema mumewe alikuwa hana kazi baada ya kuachishwa kazi kutokana na janga la COVID-19.
Hata baada ya hali kuwa shwari na mabasi kurudi njiani, alidai kuwa familia imekuwa katika wakati mgumu kwa sababu mumewe alikuwa akienda kwa miezi bila malipo.
"Katika miezi michache iliyopita tangu Februari imekuwa ngumu kwetu kwa sababu hawajalipwa tangu wakati huo. Alikuwa akirudi nyumbani kutoka kazini lakini hana pesa,” alisimulia.
Mama Mercy pia alidai mumewe hapo awali alitoa wasiwasi kuhusu breki za basi: "Amekuwa akilalamika kuhusu hali ya basi kwa muda sasa.
Alitumia muda mwingi kwenye karakana na basi hilo.”
Wakati huo huo, Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) imesitisha shughuli zote za mabasi ya Modern Coast.
Chanzo - Tuko News