Askofu wa kanisa la Kiinjili La Kilutheri Tanzania Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Dkt. Emmanuel Joseph Makala ameiasa jamii kuacha mara moja kuyanyanyasa makundi ya watu wenye ulemavu.
Askofu Makala ameyasema hayo katika mahafali ya 10 ya kuwaaga wahitimu wa mafunzo ya Ujasiriamali yaliyofanyika siku ya Jumamosi ya tarehe 16/07/2022 katika Ukumbi wa kanisa hilo usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Shinyanga yakijumuisha mabinti 12 wenye Ualbino wanaofadhiliwa na KKKT- DKMZV chini ya mradi wa RIGHT TO LIVE WITH ALBINSM katika kituo cha Wadiakonia kilichopo Mwasele Shinyanga.
"Zamani walikuwa wanafikiri kwamba hawa watu hawawezi kufanya chochote, lakini wanaweza, na zamani hawa watu hata ukifika wakati wa kuhesabiwa walikuwa wanafichwa kama vile sio watu. Sasa nichukue nafasi hii kuiasa jamii kwamba hawa ni watu kama watu wengine na wana akili wengine wanatushinda wana maadili wengine tunashindwa nao, kwa hiyo na wenyewe ni ndani ya Watanzania watakaohesabiwa", alisema Askofu Makala.
Askofu Makala aliongeza kuwa watu waache tabia ya kuwaficha wenye ulemavu, wagonjwa kwa mantiki ya kuwa nao ni watoto wa Mungu kama tulivyo wengine.
Askofu Dkt. Emmanuel Makala amewapongeza mabinti hao wenye Ualbino na kuwaomba kutumia ipasavyo maarifa yote waliyoyapata kwa walimu wao ili waweze kutimiza malengo yao.
Pia Askofu Dkt. Makala ameiomba jamii pamoja na wadau mbalimbali kushirikiana kusaidia makundi tegemezi kwasababu ni miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa utakaoweza kuisaidia jamii.
Hadi hivi sasa Dayosisi imefanikiwa kusaidia mabinti 102 wenye Ualbino kwa kuwapatia ujuzi wa aina tofautitofauti kama vile kushona nguo kwa cherehan, kutengeneza sabuni za maji, pamoja na mapishi mbalimbali.
Katibu mkuu wa Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Bi. Happy Gefi akifanya utambulisho wa wageni wakati mahafali hiyo
Wahitimu wa mafunzo ya Ujasiriamali wakiwa ndani ya ukumbi wakati wa mahafali
Kaimu Mtunza hazina wa Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria ndugu Mathias Masele akiwasilisha jambo wakati wa mahafali
Picha na
Isaac Masengwa - Masengwa Blog
Social Plugin