Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UKIKUTWA GESTI UTAHESABIWA SIKU YA SENSA



Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na wadau mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Julai 4,2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati akiendelea kutoa elimu ya Sensa na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23,2022 . Picha na Malunde 1 blog

Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Kamisaa wa Sensa ya watu na Makazi Mhe. Anne Makinda, amesema zoezi la kuhesabu Sensa mwaka huu (2022) litakuwa la kidigital na halitaruka Kaya hata moja, na watahesabu watu wote watakaolala ndani ya mipaka ya nchi ya Tanzania hadi wale ambao siyo Watanzania ikiwemo wale watakutwa wakiwa wamelala kwenye nyumba za wageni (Gesti), kwenye Stendi za Mabasi na maeneo mbalimbali.

Makinda amebainisha hayo leo Julai 4, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa dini, Serikali, Wakurugenzi, Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa, Shirikisho la vyama vya watu wenye Ulemavu, na wadau kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Amesema zoezi la kuhesabiwa Sensa la mwaka huu ni la aina yake, ambalo litafanyika tofauti na miaka yote kwa njia ya kidigitali kwa kutumia vishikwambi, na hakuna Kaya ambayo itaruka bali zote zitahesabiwa, na ikitokea kurukwa mfumo una kataa na kutoa taarifa makao makuu kuwa kuna Kaya imerukwa.

Aidha, amesema zoezi hilo la Sensa litahesabu watu wote, wakiwamo na wale ambao siyo Watanzania ambao watakutwa wakiwa wamelala kwenye nyumba za wageni (Gesti), Mipakani, pamoja na kwenye Stadi za Mabasi sababu na wao wamekuwa wakitumia huduma za hapa nchini.

“Nawasihi Watanzania tuonyeshe uzalendo katika zoezi hili la kuhesabiwa Sensa, sababu ni muhimu kwa maendeleo yetu na hakuna mtu ambaye ataachwa kuhesabiwa na tutafika hadi kwenye nyumba za kulala wageni, Magerezani, Hospitalini, na tutawahesabu hadi wageni watakaokutwa na zoezi hili wakiwa Tanzania,”amesema Makinda.

“Zoezi hili la Sensa ni kuhesabiwa mara moja tu na ninaomba wananchi mtoe ushirikiano wa kutosha kwa Makarani pamoja na kutoa taarifa sahihi, na taarifa ambazo mtazitoa zitakuwa na usiri mkubwa na Karani ambaye atatoa siri hiyo atafungwa Jela,”ameongeza.

Ametaja faida ya Sensa ni kuchochea maendeleo kwa wananchi, ambapo Serikali inataka kuwa na idadi ya watu wake kamili na kuisaidia katika kupanga mipango yake ya maendeleo kwao na kuwahudumia kulingana na idadi yao.

Katika hatua nyingine Makinda ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, amewaasa wadau hao wakiwamo viongozi wa dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kuendelea kuhamasisha wananchi washiriki kikamilifu kuhesabiwa kwenye zoezi hilo la Sensa ambalo mpaka sasa limebakiza siku 49.

Naye Mtakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Makao Makuu Pastory Ulimali, amesema taratibu zote za zoezi hilo la Sensa limeshakamilika, ambalo pia litafanyika kwa mfumo wa digitali na hakuna Kaya ambayo itaachwa kuhesabiwa, sababu Kaya ikirukwa mfumo unatoa taarifa.

Nao baadhi ya Washiriki wa kikao hicho, wamepongeza kupewa elimu hiyo ya Sensa huku wakiahidi kutoa ushirikiano wa kuhamasisha wananchi washiriki kikamilifu kuhesabiwa Sensa siku hiyo ya Agost 23 mwaka huu.

Soma zaidi hapa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com