Na Shomari Binda-Musoma
WANANCHI wameshauriwa kuwa na utamaduni wa kupima Homa ya Ini kutokana na ugonjwa huo kuwa na desturi ya kujificha.
Kauli hiyo imetolewa na daktari wa magonjwa ya binadamu,Muhamed Sadri,kutoka Royal Poly Clinick iliyopo mjini hapa wakati wa zoezi la upimaji wa bure wa ugonjwa huo.
Amesema binadamu anaweza kuishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu bila kujionyesha hivyo ni muhimu kuufanyia vipimo.
Daktari huyo amesema yapo madhara yatokanayo na ugonjwa ikiwemo vifo lakini pale unapofanya uchunguzi na kupata chanjo yake utajiepusha nao.
Amesema shirika la afya duniani ( WHO) lilipitisha kila tarehe 28 Julai kuwa siku ya Homa ya Ini ili kutoa ukumbusho na elimu ya kupambana na ugonjwa huo.
"Sisi kama Royal Poly Clinick tunaungana na serikali katika mapambano dhidi ya Homa ya Ini dhidi ya wananchi.
' Tangu julai 20 hadi 28 tunaendesha zoezi a upimaji na kutoa chanjo ya Homa ya Ini bure na kutoa ushauri wa afya", amesema Sadri.
Amesema afya ndio suala la msingi na mtu anapokuwa na afya njema anakuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kiuchumi.