Mfano wa nguo fupi
Mwenyekiti wa mtaa wa Luhende Msafiri Nadula
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Watoto watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa Miaka 12 wanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi katika Manispaa ya Shinyanga wamekamatwa kupitia serikali ya mtaa wa Luhende kata ya Maselelo Manispaa hiyo wakijihusisha na biashara ya kuuza miili yao katika eneo la mtaa wa Jomu maarufu kama Bakurutu.
Taarifa hizo zimetolewa na mwenyekiti wa mtaa wa Luhende kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga Msafiri Nadula wakati akizungumza na Mwandishi wetu ambapo amesema tukio hilo limetokea Julai 18 Mwaka huu 2022 na kwamba watoto hao walikamatwa usiku wakiwa wamevaa nguo fupi.
Mwenyekiti Nadula amefafanua kuwa watoto hao baada ya kuwakamata walikiri na kwamba alichukua hatua za kuwafikisha kituo cha Polisi ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
''Kuna wasamaria wema waliwaleta watoto wawili saa kumi usiku kwamba wamewakamata wakiwa wanadanga lakini mavazi yao waliyokuwa wamevaa ni kweli yalikuwa ya udangaji basi wakanikabidhi wao wakaondoka ikabidi niwahoji wale watoto wanaakili ni kweli nikawaambia sasa mlitoka hivi nyumbani na hizi nguo wakasema hapana tulivua hizo nguo tukaweka kwenye pagala wakanipeleka kwenye hilo pagala tukalikuta hilo furushi la hizo nguo zingine za nyumbani,"amesema.
"Nikawaambia kwa nini mnafanya namna hii mlikuwa wangapi wakasema tulikuwa watatu basi ikabidi niwapeleke polisi kwa kweli mavazi waliyokuwa wamevaa mpaka polisi walishangaa sana kwamba hiki kizazi cha wapi tena watoto wadogo miaka 11/12 wanafanya mambo ya namna hii ni kitu cha ajabu wakawahoji hoji polisi pale na kukiri walikuwa wanadanga'', amesema Nadula.
Aidha Mwenyekiti huyo amewakumbusha Wazazi, walezi na jamii wajibu wa malezi na makuzi kwa watoto ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili kwa watoto ambao baadhi yao wamekuwa wakijihusisha na utumiaji wa vilevi na biashara ya ngono.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa tabia ya watoto kujihusisha na vitendo viovu kama biashara ya ngono na utumiaji wa vilevi inachagiwa na baadhi ya wazazi wanaoshindwa kutimiza jukumu lao la kuwalea na kuwahudumia watoto.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Masekelo akiwemo Zakia Abdul wamesema mmomonyoko wa maadili kwa watoto unachangiwa na wazazi wanaokwepa jukumu la kuwalea na kuwatunza watoto wao huku akitaja chanzo cha watoto hao kujihusisha kwenye makundi mabaya.
''Chanzo cha hao watoto kulawitiwa au kuwa na maisha magumu ni mama yao mzazi kwa sababu mama yao mzazi muda wote yupo kwenye pombe hajui watoto wanakulaje wanashindaje yeye kurudi ni usiku na anakuwa anawajengea mazingira magumu kwa sababu anabadilisha wanaume kila aina kwa hiyo watoto wanaweza kuwa wanafanya uamuzi huo ili na wao waweze kupata mahitaji yao kwahiyo mimi naona kama kuna msaada unaweza kupatikana wapatikane hata ndugu hata wasamaria wema wawachukue wale watoto ili waweze kutumiza ndoto zao kwa sababu bado wadogo sana'',amesema jirani Zakia
Mmomonyoko wa maadili kwa watoto unatajwa kusababishwa na baadhi ya wazazi na walezi wanaoshindwa kufuatilia mwenendo wa watoto wao wawapo katika mazingira ya shule na nyumbani.
Social Plugin