Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LEMBELI ACHUKUA FOMU KUGOMBEA UENYEKITI CCM MKOA WA SHINYANGA


James Lembeli akiwa ameshika fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
 

Na Marco Maduhu, SHINYANGA


Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) James Lembeli amejitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga.

 Lembeli ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini kuanzia mwaka (2005-2015) kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, baadae akajiunga CHADEMA na kurudi tena CCM, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Uenyekiti CCM Mkoa wa Shinyanga leo Julai 9, 2022 katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, na kukabidhiwa na Katibu wa Chama hicho Donald Magesa.

Akizungumza wakati wa kuchukua fomu hiyo,Lembeli amesema ameamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, mara baada ya kujipima na kujitathmini na kujiona kuwa nafasi hiyo anaiweza kwa  sababu ana uzoefu ndani ya Chama, na pia ni kiongozi mzoefu ndani na nje ya nchi na anaweza kuongoza vizuri Chama.

Lembeli ambaye pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira (2010-2015),amesema Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga, kinahitaji viongozi thabiti, makini na hawana makando kando, sifa ambazo anazo na kuamua kugombea nafasi hiyo ya Uenyekiti CCM Mkoa.

“Nimejipima na kujitathmini nikaona nije nichukue fomu ili nigombee nafasi ya Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga kwa sababu sifa zote ninazo, hasa katika zama hizi ambapo kuna changamoto nyingi,” amesema Lembeli.

Makada wa CCM wameendelea kuchukua fomu za kuwania uongozi ambapo Julai 6 mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja (2007-2015) kisha akahamia CHADEMA na kurudi tena CCM, naye amechukua fomu ya kugombea tena nafasi hiyo ya Uenyekiti wa CCM Mkoa huo, uchaguzi ambao utafanyika mwaka huu.


Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Donald Magesa, amesema idadi kamili ya wagombea wote ambao wamechukua fomu ataitaja kesho siku ya hitimisho la uchukuaji fomu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com